……………….
Mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa zimeanza mkoani Katavi ambapo zitakimbia umbali wa kilometa 910.5 na kutembelea jumla ya miradi 43 yenye thamani ya shilingi bilioni 11.8.
Mbio hizo zimepokelewa kutoka mkoani Rukwa na kuanza kukimbizwa katika Halmashauri ya Mpimbwe na kukagua miradi mbalimbali yenye jumla ya thamani ya shilingi 5.1 na kuweka mawe ya msingi katika miradi huku miradi mingine ikizinduliwa.
Katika shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyopo katika halmashauri hiyo Mwenge wa Uhuhu umeweka jiwe la msingi katika mradi wa nishati safi ambapo shule hiyo itaondoa matumizi ya nishati chafu wakati kupika chakula cha wanafunzi kufuatia kuanza kupika kwa kutumia kwa nishati safi ya gesi hali itakayopunguza ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.
Aidha shule hiyo pia imeendelea kupanda miche ya miti ili kuboresha mazingira.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa bwana Godfrey Mnzava ameitaka jamii kuendelea kuyatunza mazingira ili kuepuka mabadiliko ya tabia nchi.
Katika mradi mwingine jumla ya wakazi 34,650 wa vijiji vitano vya Usevya, Minyoso, Ikuba, Nyambwe na Msadya wameanza kunufaika na mradi mkubwa wa maji safi uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.26.
Akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wilaya ya Mlele mhandisi Charles Mengo amesema mradi huo una mtandao wa kilometa 79 na una tanki la ujazo wa lita milioni moja na laki mbili.
Alieleza kuwa kabla ya mradi huo wananchi walilazimika kuchota maji katika visima na pampu za maji.
Mbunge wa jimbo la Kavuu Geophrey Pinda alisema mradi huo wa maji umeinua mji wa Usevya.
“Maji haya yanatoka katika milima ya Lyamba na yanakuja mpaka huku kwa wananchi. Kwa kweli tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan” alisema Pinda.
Mradi huo umezinduliwa rasmi na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa bwana Godfrey Mnzava na amewataka wananchi kuutunza.