Na Sophia Kingimali.
BARAZA la Taifa la mitihani (NECTA) limetoa rai kwa wadau wote wa elimu nchini kushiriki katika kudhibiti vitendo vyovyote vya udandanyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wa mwaka 2024 unaotarajiwa kuanza kesho Septemba 11,2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10,2024 jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt Said Mohamed amesema jumla ya watahiniwa waliosajiliwa 1,230,780 wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
“Kati ya watahiniwa 1,230,780 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka 2024,watahiniwa 1,158,862 ambao sawa na asilimia 93.16 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili na watahiniwa 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya kwa lugha la Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunza”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu ambao wamesajiliwa kwenye mtihani huo 4,583 kati yao wasioona 98,uoni hafifu 1,402, wenye uziwi 1,067wenye ulemavu wa akili 486 na wenye ulemavu wa viungo ni 1,530.
Amesema mpaka sasa maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo.
“Pamoja na maandalizi yote kukamilika nitoe rai kwa kamati zote za mitihani za Mikoa na Halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vyote vya mitihani unaimarishwa na vituo hivyo vinatumika kwa kuzingatia Mwongozo uliotolewa na Baraza la Mitihani Nchini”,Amesema Dkt Mohamed.
Sambamba na hayo NECTA imewataka watahiniwa kufanya mtihani huo kwa kuzingatia kanuni za mitihani hivyo baraza hakitarajii kuona mwanafunzi yeyote anajihusisha na vitendo vya udandanyifu kwani atakayebainika kufanya vitendo hivyo matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa sheria.
Pia, NECTA imewataka wasimamizi wa mitihani hiyo kufanya kazi hiyo kwa uadilifu na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake.
“Wasimamizi wahakikishe watahiniwa wenye mahitaji maalum wanafanya mitihani yao ipasavyo ili wapate haki yao ya msingi,pia watahiniwa wenye mahitaji maalumu waongezewe muda dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine”,Amesema.