Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Septemba 9,2024
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ally Hapi, mkoani Pwani, amewasisitiza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM pamoja na wananchi kijumla kuendelea kuwaunga mkono viongozi waliopo madarakani, wabunge na madiwani hadi wamalize ngwe yao ya uongozi kabla ya uchaguzi mkuu ujao,(2025).
Vilevile amesisitiza umuhimu wa mshikamano ndani ya chama na kuepuka mipango ya mapema ya kujipitisha kwa lengo la kugombea kabla ya wakati wa uchaguzi.
Akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Kibaha, Bagamoyo na Mkuranga Hapi alionya dhidi ya wapambe na madalali ambao wanaweza kuvuruga chama kwa kuanza kujipendekeza au kuwakatisha tamaa viongozi waliopo madarakani.
Aidha, Hapi alihimiza wanachama kuendelea kuisemea CCM kwa mafanikio makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hususan kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kimkakati.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kiongozi wa kielelezo hapa nchini kwa kutoa pesa nyingi za miradi ya maendeleo kila kona ya nchi hii, kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati,twende tukayaseme haya”
“Tusichukue muda mwingi kujitambulisha na kujisifia muda wa kujisifia tuutumie kuisemea ilani ya Chama ilivyotekelezwa”
Vilevile Hapi aliwataka waache kufanya kazi kwa mazoea kwani hakuna muda wa kuchezea kwasasa.
Kadhalika Hapi aliwataka wanachama wa CCM, kuwa na mshikamano kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 2024 na kuongeza idadi ya wanachama kwani ndio mtaji wa chama.
Awali Mbunge wa Jimbo la Chalinze (Waziri)Ridhiwan Kikwete alihimiza wananchi kujiandikisha kwenye daftari la ukaazi na kupiga kura ambapo sanjali na hilo amewasihi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya.
Mwenyekiti wa CCM Mkoani Pwani Mwinshehe Mlao, alimhakikishia Hapi kwamba ,CCM Mkoani Pwani ipo imara na imejipanga kupata ushindi kuanzia uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 2024 na uchaguzi mkuu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa,Hapi alianza ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Pwani septemba 6 na kukamilisha ziara hiyo wilayani Rufiji septemba 9 mwaka 2024.