Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumzia Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika ambapo Tanzania ni miongoni kwa nchi zinazonufaika pakubwa na uhusiano huo uliokita mizizi.
…………………
Katika mkutano wa jukwaa la ushirikiano kati ya Afrika na China uliofanyika nchini China hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametoa taarifa muhimu kuhusu maeneo kumi yaliyopatiwa kipaumbele na serikali ya China kupitia Rais wake. Profesa Mkumbo ameeleza kuwa maeneo hayo yamelenga kuleta maendeleo nchini Tanzania, huku yakihusisha sekta za elimu, viwanda, uwekezaji, miundombinu, na biashara.
“Maeneo haya yapo ndani ya ajenda ya kuleta maendeleo Tanzania kupitia nyanja zote. Rais wa China ametangaza kufungulia soko la biashara la China kwa ajili ya bidhaa kutoka Tanzania, na hakuna bidhaa itakayotozwa ushuru. Hii ni fursa kubwa na haijawahi kutokea duniani,” amesema Profesa Mkumbo.
Aidha, ameongeza kuwa soko la China ni kubwa sana kwa bidhaa za Afrika, ikiwemo Tanzania, na kwamba serikali itaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia nafasi hiyo. “Fursa hii ni ya kipekee kwa Watanzania, hasa kwa kuzingatia ukubwa wa soko la China,” aliongeza.
Katika maelezo yake, Profesa Mkumbo pia amezungumzia msaada wa kifedha ambao Tanzania itanufaika nao kupitia dola za Kimarekani bilioni 50 zilizotengwa ambazo ni sawa na takriban shilingi trilioni 135 za Kitanzania. Fedha hizo zimegawanywa katika makundi matatu, ambapo dola bilioni 29 zitapokelewa kama mikopo, dola milioni 11 zitakuwa kwa njia ya msaada, na dola bilioni 10 zitatumika kwa uwekezaji wa makampuni ya China nchini Tanzania.
“Fedha hizi ni nyingi sana. Tayari nimeagiza Tume ya Mipango ifanyie kazi haraka mpango huu, kwa kuwa ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi,” amesema Profesa Mkumbo, huku akiongeza kuwa Tanzania isipochukua hatua za haraka, fursa hiyo itapotea na fedha hizo zitapelekwa sehemu nyingine.
Profesa Mkumbo pia ameagiza Kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania kuhakikisha angalau theluthi moja ya hizo dola bilioni 10 zinatumiwa na makampuni ya China kuwekeza nchini.
Amefafanua kuwa tayari hatua zimeanza, na Rais wa Tanzania anakutana na baadhi ya wawekezaji wakubwa kutoka China ili kufanikisha malengo hayo.
“Rais amekutana na wawekezaji wakubwa, na tunaamini hii ni fursa kubwa kwa Tanzania,” amesema Profesa Mkumbo.
Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na China, Profesa Mkumbo amebainisha kuwa kila eneo la maendeleo nchini limeguswa na serikali ya China, na sasa ni wakati wa Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo.
“Kushindwa kutumia fursa hizi itakuwa hasara kubwa kwa nchi yetu, huku mataifa mengine yakiendelea kufaidika,” ameongeza.
Pia ameonya kuwa endapo Watanzania watashindwa kutumia fursa hii, mataifa 53 ya Afrika yatapata faida kubwa, huku Tanzania ikibaki nyuma. Alisisitiza kuwa kama viongozi hawatakubaliana na hilo, kwani Rais wa Tanzania ameleta heshima kubwa kwa nchi kwa jinsi alivyoshiriki katika mkutano huo.
“Ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyozungumza vizuri katika mkutano huu akiwakilisha Afrika Mashariki. Hotuba yake imepokelewa kwa furaha, na ameiheshimisha nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla,” amemalizia ProfesaMkumbo.