Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar akizungumzia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini China hivi karibuni.
……………………..
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na China unaosimamiwa na viongozi wa juu wa nchi hizo mbili, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Xi Jinping wa China, unazidi kuimarika, hasa katika nyanja za biashara, viwanda, kilimo, na utalii.
Akizungumza wakati wa mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Tanzania na China lililofanyika nchini China, Balozi Omar amesema jukwaa hilo lilifanyika katika ngazi tatu tofauti—maofisa wa ngazi ya chini, mawaziri, na wakuu wa nchi na serikali kutoka Afrika na China. Ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China ulianza rasmi mwaka 1964 chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na kufikia mwaka huu wa 2024, mataifa hayo yamesherehekea miaka 60 ya ushirikiano wa karibu.
Balozi Omar amefafanua kuwa ushirikiano huu umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili, na sasa Tanzania ina nafasi ya kuwa mfano bora wa ushirikiano wa kimkakati barani Afrika.
“Tumepata mafanikio katika mzunguko wa kwanza wa ushirikiano wetu, na sasa tunapoingia kwenye mzunguko wa pili, tunategemea mafanikio makubwa zaidi.
China imeweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta za uchumi, uwekezaji, biashara, viwanda, na uchakataji wa madini,” alieleza Balozi Omar.
Kuhusu biashara kati ya Tanzania na China, Balozi Omar amesema mwaka 2023, biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia thamani ya dola bilioni 8.7.
Aliongeza kuwa China imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji binafsi nchini Tanzania, na kuwa mshirika mkubwa wa kiuchumi kwa nchi hiyo.
“Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa kimbilio la wawekezaji binafsi, na tumeshuhudia ongezeko la mitaji ikija Tanzania. Pia, ushirikiano wetu unahusisha sekta ya elimu, ambapo Watanzania wengi wanasoma nchini China bila changamoto yoyote,” alisema.
Balozi Omar pia amezungumzia ushirikiano wa kiutalii, akieleza kuwa idadi ya watalii wa Kichina wanaotembelea Tanzania imekuwa ikiongezeka, ingawa bado si kubwa sana.
Alisisitiza kuwa uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China umepelekea kubadilishana kwa viongozi wa ngazi za juu, huku akitaja ziara za viongozi toka enzi za Mwalimu Nyerere hadi sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Viongozi wa nchi hizi mbili wamekuwa wakitembeleana mara kwa mara, jambo ambalo linaonyesha dhamira ya kuendeleza makubaliano ya kimkakati katika nyanja zote muhimu, ikiwemo biashara, elimu, utalii, na uongozi,” amehitimisha Balozi Omar.