*Wawekezaji waonesha nia kuwekeza kwenye biashara ya uwindaji wa kitalii na hoteli nchini.
Na. Mwandishi wetu, Abu Dhabi.
Maonesho ya Kimataifa ya Uwindaji wa Kitalii yanayojulikana kwa Jina la “Abu Dhabi International Hunting and Equestrian Exhibition – ADIHEX 2024” yamezaa matunda kufuatia idadi kubwa ya wawekezaji waliohudhuria katika maonesho hayo yaliyoanza tarehe 31 Agosti hadi 08 Septemba, 2024 kuonesha nia ya kuwekeza nchini.
Miongoni mwa mafanikio ya maonesho hayo ni mazungumzo mahsusi yaliyofanywa baina ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Mabula Misungwi Nyanda na wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza kwenye biashara ya uwindaji wa kitalii, ujenzi wa hoteli za kulala watalii ndani ya Hifadhi na uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA) mazungumzo yaliyoongozwa na Kaimu Balozi wa Tanzania katika nchi za umoja wa falme za kiarabu Bw. Hangi L. Mgaka.
Bw. Hangi Mgaka ameipongeza TAWA kwa ushiriki wake kwenye maonesho hayo ambayo kwasasa ni mara ya tatu tangu Taasisi hiyo ianze kushiriki mwaka 2022, maonesho yanayotajwa kukutanisha zaidi ya washiriki 170,000 Kila mwaka.
Aidha katika kufikia masoko makubwa katika nchi za Mashariki na Kati, Kaimu Balozi huyo amesisitiza kuwa TAWA iendelee kushiriki makongamano mbalimbali yanayofanyika katika falme za kiarabu ikiwa ni pamoja na nchi za Saudi Arabia na Bahrain.
Vilevile ametoa wito kwa Kampuni za uwindaji wa Kitalii kutoka Tanzania kushiriki maonesho hayo ili kupata wageni watakaokuja nchini kwa shughuli za uwindaji wa kitalii na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
TAWA inashiriki maonesho haya kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji kwenye maeneo inayoyasimamia ikiwemo uwindaji wa kitalii na utalii wa picha na maeneo ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA).