06 Septemba 2024, Dar es Salaam: Wahandisi nchini wamekumbushwa umuhimu wa huduma za hali ya hewa sambamba na kuchangia gharama za upatikanaji wa huduma hiyo katika utekelezaji wa miradi yao.
Hayo yalizungumzwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa katika mada iliyowasilishwa katika Mkutano wa 21 wa Wahandisi uliyojumuisha wahandisi wa ndani na nje ya nchi katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, tarehe 05 hadi 06 Sepetemba, 2024.
Dkt. Kabelwa alieleza kuwa, katika hotuba ya Waziri wa Fedha ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2024/25, kifungu cha 158 ilijumuisha mapendekezo ya mabadiliko ya kufanya marekebisho ya sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, sura 157 kuhusu Ada za Hali ya hewa kwa usalama wa uendeshaji wa miradi ya ujenzi.
“Lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato yatakayowezesha utoaji wa huduma mahsusi za hali ya hewa ili kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi na kuimarisha usalama wa watu na mali katika maeneo ya miradi ya ujenzi, ambapo mchakato wa upatikanaji wa huduma hizo unahitaji uwekezaji wa miundombinu ya kisasa na gharama kubwa za uendeshaji”. Alifafanua Dkt. Kabelwa.