Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Taifa ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Ijumaa Septemba 06, 2024, amefanya Mkutano Maalum na Waandishi wa Habari, hapo katika Ukumbi wa Golden Tulip Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.
Mkutano huo umelenga Kutangaza Baraza Jipya Teule la Mawaziri Kivuli wa Chama hicho, kwa Upande wa Zanzibar.
Uwepo wa Baraza hilo ni kwamujibu wa Miongozo ya Katiba ya Zanzibar, inayopendekeza kuwepo kwa ‘Sauti ya Wananchi kupitia Upande wa Upinzani, pamoja na Matakwa ya ile ya ACT-Wazalendo, inayoelekeza kuundwa kwa Chombo hicho Wasemaji wa Sekta mbali mbali za Maendeleo ya Nchi, kupitia Kambi hiyo.
Akitoa Hotuba yake kabla kutangaza Viongozi walioteuliwa Kuongoza katika Baraza hilo, Mheshimiwa Othman amesema uteuzi huo umezingatia taaluma, weledi katika eneo husika, maarifa na uzoefu, kwa kuzingatia Sera za Sasa za Chama na Ahadi zake (The Brand Promises), pamoja na kuzitambua na kuzitatua changamoto za wananchi.
“Moja ya kazi za Baraza hili, ni kusimamia utendaji wa Serikali kwa ukaribu na ufanisi zaidi pamoja na kusimamia maslahi ya Wananchi”, amesema Mheshimiwa Othman.
Aidha amesema wameamua kutangaza Baraza hilo muda huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, wakiamini kwamba watakiwakilisha vyema Chama kuwa Sauti kubwa ya wananchi.
Viongozi mbali mbali wamejumuika katika hafla hiyo wakiwemo Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Ndugu Ismail Jussa Ladhu; Naibu Katibu Mkuu upande wa Zanzibar, Ndugu Omar Ali Shehe na Katibu wa Habari Uenezi na Mahusiano ya Umma, Ndugu Salum Bimani.
Tangazo hilo limekuja baada ya Vikao vya Halmashauri na Kamati Kuu za Chama hicho, kufuatio Agizo na Mapendekezo ya Kiongozi wa Chama, Bi. Doroth Semu, ambaye ndiye mwenye Mamlaka ya Kisheria, kwamujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo, inayomuelekeza kufanya Uteuzi wa Wasemaji hao wa Sekta zipatazo 16.