Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .ZAIDI ya wananchi 1000 wanatarajiwa kushiriki mbio za SHANGILIENI Marathon msimu wa pili ambazo zimekuwa zikiandaliwa mahususi kwa ajili ya kuimarisha Afya na kusaidia jamii iliyopo pembezoni kwa kuchangia huduma ya afya .
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mratibu wa SHANGILIENI MARATHON, Scolastica Porokwa Porokwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mbio hizo.
Amesema wamelenga kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia jamii ambazo hazifikiwi kirahisi Kwa kupeleka huduma za Afya yakiwemo madawa vyakula na mavazi hasa jamii ya Wahadzabe iliyopo wilayani Karatu.
“Kiingilio katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika September 14,ni shilingi 35,000 na katika fedha hizo utapewa tisheti na medali pamoja na zawadi mbalimbali na fedha hizo zitakwenda Kusaidia jamii ya pembezoni hususani wahadzabe “amesema Porokwa.
Amesema kuwa mashindano hayo ya Shangilieni Marathon katika msimu uliopita mwaka jana 2023 yalikuwa na mafanikio makubwa baada ya kuwafikia jamii ya pembezoni zaidi ya 800 na akina mama 400 walipatiwa huduma bure za kiafya.
“Mbio zetu zitakuwa kati ya kilometa 5 hadi 21 na washiriki watapata huduma zote stahili hivyo natoa wito kwa watu mbalimbali kushiriki kwa wingi katika mbio hizo ili kuweza kufanya mazoezi hayo sambamba na kusaidia kuwaunga mkono jamii hizo zenye changamoto “amesema Porokwa.
Kwa upande wake Meya wa jiji la Arusha Maxmilian Iranghe amewataka wakazi wa jiji la Arusha na viunga vyake, kujitokea kushiriki mbio za SHANGILIENI Marathon ambazo zimekuwa zikiandaliwa mahususi kwa ajili ya kuimarisha Afya na kusaidia jamii iliyopo pembezoni kwa kuchangia huduma ya afya .
Amesema mbio hizo za SHANGILIENI MARATHON ni msimu wa pili kuandaliwa na kanisa la Anglikana, huku akiitaka jamii kuwa wajibu wa kushiriki mbio hizo kama sehemu ya kujikinga na maradhi nyemelezi, zinazotarajiwa kufanyika September 14,2024.