Katika jua la jioni lililokuwa likizama jijini Dar es Salaam leo Septemba 6, 2024 wahandisi kutoka pande zote za nchi na nje ya nchi walikusanyika kwa ajili ya kilele cha kufunga siku ya wahandisi, tukio lililojaza matumaini ya mustakabali bora wa fani ya uhandisi nchini Tanzania.
Mkutano huu wa mwaka, wa 21 tangu uanze, umefanyika katika ukumbi Mlimani City uliosheheni mawazo na ndoto za wahandisi vijana, wazee, na wadau mbalimbali wanaoshirikiana kukuza sekta hii muhimu.
Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Waziri wa Ardhi na Maendeleo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Rahma Kassim Ali, aliwasilisha salamu za serikali, akisisitiza dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza, kuilinda, na kuendeleza fani ya uhandisi.
Aliweka wazi kwamba uhandisi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa, hususan katika nyanja za mapinduzi ya kiteknolojia ya ujenzi.
Akihutubia kwa hisia kali, Rahma Kassim Ali aliwahimiza wahandisi kuunga mkono mpango wa mradi wa STEAM, mradi wenye malengo ya kuhamasisha vijana kujiunga na sekta ya uhandisi kwa vitendo.
“Tunawahitaji vijana katika uwanja huu, kwa sababu wao ndiyo watakaosukuma mbele teknolojia za kesho,” alisisitiza Waziri Rahma, akizidi kueleza umuhimu wa kuandaa kizazi kipya cha wahandisi wenye ubunifu na uthubutu.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Bernard Kavishe, alipata nafasi ya kuchambua zaidi kuhusu hatua zinazochukuliwa na bodi yake katika kukuza taaluma ya uhandisi, akieleza kwamba bodi imejizatiti kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wahandisi wanapata mazingira bora ya kufanya kazi na kuboresha ujuzi wao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education, AbdulMalik Mollel, aliongeza kwamba taasisi yake ipo tayari kushirikiana na Bodi ya Wahandisi Tanzania ili kutoa fursa za elimu na ujuzi bora katika vyuo vya nje ya nchi itakayowasaidia wahandisi vijana kuwa na maarifa sahihi katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia. “Tunaamini kwamba kwa kutoa elimu bora, tutawawezesha wahandisi wetu kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” amesema Mollel kwa kujiamini.
Naye Dkt. Kisenge, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), aliweka msisitizo kuhusu mchango wa wahandisi katika sekta ya afya, hasa kwenye maendeleo ya vifaa tiba na miundombinu ya kisasa inayosaidia kuboresha huduma za afya nchini. Aliahidi kushirikiana na bodi hiyo kwa karibu ili kuhakikisha fani ya uhandisi inazidi kukua.
Kadri mkutano ulivyokuwa unafikia mwisho, matumaini yalikuwa yamezidi kuchipuka. Wahandisi waliondoka wakiwa na ari na morali mpya, wakifahamu kwamba serikali na wadau wako tayari kuwasaidia ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi. Siku hii ambayo imeshirikisha wahandisi waalikwa kutoka nchi za Kenya, Ethiopia, South Sudan Korea China na Uganda imekuwa sio tu sherehe ya taaluma, bali pia ahadi ya kesho iliyojaa mafanikio kwa Tanzania kupitia uhandisi.