Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 za maji lililojengwa katika mradi wa maji Mbangamao uliotekelezwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya Sh.bilioni 1.7.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhandisi Mashaka Sinkaka wa pili kushoto akielezea kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maj Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,wa kwanza kushoto Afisa mahusiano Ruwasa mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo.
………….
Na Mwandishi maalum. Mbinga
ZAIDI ya wakazi 3,600 wa kijiji cha Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,wameondokana na adha ya huduma ya maji safi na salama baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhandisi Mashaka Sinkala alisema,mradi huo umegharimu Sh.bilioni 1.8 ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2022 kwa sasa umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho.
Sinkala alisema,kwa sasa mradi huko kwenye matazamio ya mwaka mmoja na kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa chanzo(Intake),ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 200,000 kulaza bomba za kusambaza maji urefu wa kilometa 39,kujenga vituo 29 vya kuchotea maji na vituo 2 vya kupunguza kasi ya maji yanayotoka kwenye Tenki.
“Katika kipindi hiki cha matazamio kulitokea changamoto ndogo ya kuachia kwa viungo sehemu ya kilometa moja kwenye njia kuu ya kuingizia maji kwenye tenki na tayari tumefanyia kazi kwa kufunga vifaa vipya na sasa maji yanafika kwenye tenki na wananchi wanapata huduma kama kawaida”alisema Sinkala.
Kwa mujibu wa Sinkala,wanaendelea kuboresha huduma kwa kufunga mabomba ili kupanua mtandao wa huduma ya maji katika kitongoji cha Kilombero na Mkonde Beach ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mkazi wa kijiji hicho Roda Komba,ameishukuru Ruwasa kwa kumaliza changamoto ya maji katika kijiji hicho kwani hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji yanayopatikana kwenye visima vya asili.
Alisema,awali changamoto ya maji katika kijiji hicho ilikuwa kubwa na kusababisha baadhi ya wananchi kushindwa kushiriki katika kazi za maendeleo.
Fabinga Kapinga,ameiomba Ruwasa na Mkandarasi kutafuta suluhisho ya kudhibiti kukatika mabomba mara kwa mara ili wananchi wawe na uhakika wa kupata huduma ya maji masaa 24.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Patius Sangana,awali kulikuwa na mradi wa maji ya visima uliojengwa na taasisi moja ya dini,lakini kutokana na idadi kubwa ya watu mradi huo haukuweza kutosheleza mahitaji.
Alisema,kujengwa kwa mradi wa maji ya bomba chini ya Ruwasa,umesaidia sana kumaliza kabisa tatizo la maji kwa wananchi ambao kwa sasa wanapata muda mwingi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Sangana,amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kumaliza changamoto ya maji chini ya Kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani iliyoosaidia sana kuharakisha maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.