Na Sophia Kingimali.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na African CDC pamoja na Shirika la watoto Duniani UNICEF wamekutana kujadili namna watakavyoweza kuweka mipango yao ya ufadhili katika rasilimali fedha na eneo la kiufundi katika kuwezesha huduma ya afya ngazi ya jamii inaimarika nchini.
Akizungumza leo Septemba 3,2024 jijini Dar se salaam Afisa mpango huduma za afya ngazi ya jamii kutoka wizara ya Afya Dk.Meshack Chinyuli amesema wana Mpango kabambe wa kitaalamu ili kuwezesha utekelezaji wa mpango jumuishi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Aidha Dkt.Meshack amesema katika kikao hiko cha siku nne watajadili kwa pamoja wote ili mwisho wa siku waje na mpango wa pamoja ambao ni harakishi utakao wawezesha kutekeleza katika kutoa huduma zenye ubora ,tija na kasi inayohitajika.
Mpango huu unampango wa kuwaweka wahudumu ngazi ya afya 137,000 huku kila kijiji na kitongoji watapata wahudumu ngazi ya jamii wahudumu wawili na kwa mjini kila mtaa utakuwa na wahudumu ngazi ya jamii wawili”,Amesema.
Kwa upande wake Dr. Salim Slim Mkurugenzi huduma za kinga wizara ya Afya serikali ya mapinduzi Zanzibar amesema kuwekeza wahadumu wa afya ngazi ya jamii kutabadilisha mwenendo wa utoaji huduma huku wakiwezeshwa na kupatiwa stahiki nzuri kwa wakati ili atekeleze wajibu wake kwa wakati.
Amesema watoa huduma ngazi ya jamii ni watu muhimu hivyo kuwawezesha vizuri na kuwapa mafunzo ya kutosha kutasaidia kupunguza vifo vingi vinavyotokana na maradhi.
“Tukiweza kuwawezesha hawa watoa huduma ngazi ya jamii itasaidia watu wengi kupata huduma kwenye vituo vyetu vya afya,zahanati na Hospitali mapema kabla matatizo hayajawa makubwa na ndioo maana mpango wa Serikali zote mbili SMZ na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano kuhakikisha hawa watoa huduma wabapatikana kuanzia ngazi ya vitongoji”,Amesema.
Nae Barnabas Yesoah Community Health Specialist Africa CDS amesema wao wameamua kushirikana na serikali ya Tanzania na Zanzibar kutoa huduma katika kada ya afya ya jamii na kukuza ushirikano kwani jamii imekuwa ikisumbulia na magonjwa kuliko vitu vingine na kupelekea kupunguza nguvu kazi kutokana na kudhohofika na maradhi.
Kwa upande wake Dk. Urika Baker Daktari wa UNICEF Tanzania amesema wanatamani kuwe na mwelekeo mpya kwenye sekta ya afya na kukuza ushirikano mzuri baina ya wao na nchi.
“Tunatamani kuwe na muelekeo mpya ili tuweze kukuza sekta ya afya kuanzia ngazi ya jamii kwani itasaidia kudhibiti magonjwa mengi na kusaidia watu kupata huduma za afya mapema kabla matatizo yao hayajawa makubwa”,amesema.
Mkutano huo ni mpango kabambe wa kitaalamu ili kuwezesha utekelezaji wa mpango wa huduma za afya ngazi ya jamii umeanza leo Leo na unatarajiwa kutatamatika siku ya Ijumaa na umekutanisha wadau mbalimbali kutoka kwenye sekta ya afya kutoka ndani na nje ya nchi lengo ni kuhakikisha huduma ya afya kwa ngazi ya jamii inapewa msukumo mkubwa na kuwawezesha watoa huduma hao kwa ngazi ya jamii.