Prof. Penina Mlama Mmoja wa Waratibu wa Kamati ya Tuzo za Uandishi wa Ubunifu za Julius Kambarage Nyerere akizungumza na waandishi wa habari wakati akizungumza kuhusu tuzo hizo mwaka huu wa 2024.
…………………
Waratibu wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wameongeza nyanja yaTamtilia katika tuzo za Mwaka 2024 – 2025 ambayo ni ya Tathimilia za Jukwaani za Redio na Runinga na kufanya tuzo hizo kuwa nne kwa mwaka huu.
Akizungumza leo Septemba 3, 2024 katika Mkutano uliofanyika Taasisi ya Elimu ya Tanzania Mwenge Jijini Dar Es Salaam Prof. Penina Mlama Mmoja wa Waratibu wa Kamati ya Tuzo hiyo amesema Mwaka 2023 ilihusisha nyanja mbili za Uandishi Bunifu ambazo zilikuwa Riwaya na Ushairi
“Mwaka 2023- 2024 iliongezeka nyanja ya Hadithi za Watoto na mwaka huu imeongezeka nyanja ya Tamthilia, kwahiyo nyanja zinazoshindaniwa mwaka huu Zipo nne, ushairi, Riwaya, Hadithi za Watoto na Tamthilia “Amesema Prof. Penina.
Aidha wametaja vigezo vya kuwania Tuzo hiyo mshiriki lazima awe Mtanzania, andiko la mshiriki liwe kwa Lugha ya Kiswahili, mwandishi anaruhusiwa kuandika andiko Bunifu moja tu katika nyanja atakayo ichagua, sehemu yoyote ya Mswada isiwe imechapishwa na Mchapishaji na pamoja na kuchapishwa Mtandaoni na kwenye Magazeti au kurushwa katika vyombo vya Habari au kuonyeshwa Jukwaani.
“Wakati wa kuwasilishwa Muswada Mwandishi atatakiwa kusaini tamko Maalum kuthibitisha kuwa kazi anayo iwasilisha ni ya kwake na haijawahi kuchapishwa mahali popote, waandishi wa kwanza hadi wa tatu wa Tuzo hii wa miaka iliyopita hawaruhusiwi kushiriki kwenye nyanja yoyote ile kwa kipindi cha Miaka miwili kuanzia mwaka alioshinda”
Ameongeza kuwa miswada ilianza kupokelewa tangu kufunguliwa kwa dirisha tarehe 15 Agosti 2024 hadi tarehe 31 Novemba 2024.
Awali Prof. Penina amewakumbusha Watanzania kuwa huu ni Mwaka wa tatu wa Utoaji wa Tuzo hizo ambazo zilianzishwa mwaka 2022/ 2023.
“Kama tunavyofahamu Tuzo hii ilianzishwa na Serikali chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na inaratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania” alisema Prof. Penina.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt.Aneth Komba ambayo ndio inaratibu Tuzo hiyo ameeleza kuwa, TUZO hiyo ilianzishwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ameeleza lengo likiwa ni kuongeza rasilimali za vitabu na kuwezesha wanafaunzi nchini kupata maandiko mengi ya kusoma na kupata ari ya kusoma vitabu ambayo imepungua.
Washindi katika tuzo hizo watakabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo, mshindi wa kwanza atapata Shilingi milioni 10, Muswada wake utachapishwa na Serikali na kusambazwa shuleni na maktaba za taifa, Ngao na Cheti. Huku mshindi wa pili atapata zawadi Shilingi milioni 7 na cheti, mshindi wa tatu atazawadiwa Shilingi milioni 5 na Cheti
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Dk. Aneth Komba akifafanua jambo katika mkutano huo kati ya taasisi hiyo na waandishi wa habari.
Picha ya pamoja