Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akipata maelezo kutoka kwa Jumla Boma Mkurugenzi wa kampuni ya HEBO wakati alipotembelea mabanda kwenye kongamano la Bodi ya usajili wa Wakandarasi ERB Sam Nujoma jijini Dar es Salaam leo Septemba 3, 2024 Katikati ni Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said.
Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said akizungumza katika kongamano hilo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akizungumza katika kongamano hilo.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Bernard Kavishe akizungumza na Wahandisi vijana katika kongamano hilo lililofanyika leo Septemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam.
…………………
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amezitaka Taasisi za umma ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuwa daraja la kuwasaidia vijana kupata fursa mbalimbali kupitia taaluma zao.
Akizungumza leo Septemba 3, 2024 wakati akifungua kongamano la Wahandisi Vijana (Youth in Engeneerig Forum 2024) lililofanyika katika Ukumbi wa PSSSF Barabara ya Sam Nujoma Mwenge jijini Dar es Salaam, Mhe. Katambi, amesema kuwa lengo la serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana ikiwemo kupata ajira ndani na nje ya nchi.
Mhe. Katambi amesema kuwa Serikali imekuwa na utamaduni kwa kutoa fursa kwa wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
“Tunapotoa ajira kwa wageni tunawapa muda maalamu ili kulinda ajira za watanzania na tunapowapa kazi wanashirikiana na wazawa ili waweze kujifunza” amesema Mhe. Katambi.
Amefafanua kuwa baada ya mabadiliko ya sera, serikali ilianzisha program ya ukuzaji ujuzi ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24 wameweza kuwafikia vijana 141,160.
Ameeleza kuwa pia vijana 22,206 wamepata ujuzi nje ya mfumo rasmi ambao umewasaidia vijana wa kitanzania na kufikia malengo yao.
Mhe. Katambi amesema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa bilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ili kuwezesha miradi ya vijana 54.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde, amesema kuwa Wizara ya Ujenzi itaendelea kuunga juhudi zinazofanya wahandisi katika Taifa la Tanzania.
Dkt. Msonde ameupongeza utendaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa kuandaa Kongamano wahandisi vijana na kutoa fursa ya kuanzisha makampuni ya ujenzi.
“Tunafanya kazi kubwa ya kuwasaidia wahandisi vijana ili waweze kutatua changamoto za ujenzi pamoja na kuwahamasisha kutumia fursa zilizopo nchini” amesema Dkt. Msonde.