Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza jambo wakati akizindua kadi Janja na Mageti kwa ajili ya matumizi ya abiria wakati wanatumia Mabasi ya Yaendayo Haraka uliyofanyika leo Septemba 2, 2024 katika Kituo cha Mabasi ya Yaendayo Haraka Kimara Mwisho.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Mabasi ya Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Florens Turuka akizungumza jambo wakati uzinduzi wa kadi Janja na Mageti kwa ajili ya matumizi ya abiria wakati wanatumia Mabasi ya Yaendayo Haraka uliyofanyika leo Septemba 2, 2024 katika Kituo cha Mabasi ya Yaendayo Haraka Kimara Mwisho.
Mtendaji Mkuu Wakala wa Mabasi ya Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Athuman Kihamia akizungumza jambo wakati wa uzindua kadi Janja na Mageti kwa ajili ya matumizi ya abiria wakati wanatumia Mabasi ya Yaendayo Haraka uliyofanyika leo Septemba 2, 2024 katika Kituo cha Mabasi ya Yaendayo Haraka Kimara Mwisho.
Picha za matukio mbalimbali katika uzindua kadi Janja na Mageti kwa ajili ya matumizi ya abiria wakati wanatumia Mabasi ya Yaendayo Haraka uliyofanyika leo Septemba 2, 2024 katika Kituo cha Mabasi ya Yaendayo Haraka Kimara Mwisho.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua Kadi Janja na Mageti janja kwa ajili ya kununua na kuhakiki tiketi kwa ajili ya matumizi ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka jambo ambalo litasaidia kuondoa changamoto ya foleni ya ununuzi wa tiketi katika vituo vya mwendokasi.
Akizungumza leo Septemba 2, 2024 katika hafla ya uzinduzi kadi Janja na Mageti janja kwa ajili ya kununua na kuhakiki tiketi za usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Kimara, Mhe. Mchengerwa ametoa pongezi kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Kamati ya Bunge kuhusu kuachana na tiketi za karatasi.
“Dhamira ya Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha tumeboresha usafiri wa umma wa mabasi ya mwendokasi katika Jiji la Dar es Salaam kwa kumaliza changamoto zote za abiria kabla ya kwenda kwenye mikoa mingine” amesema Mhe.Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa watumishi wa DART pamoja na watoa huduma wake kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kujibu hoja za abiria kwenye mradi wa DART.
Amesema kuwa ni muhimu DART kujipanga kikamilifu ili kuhakikisha kadi janja zinapatikana kwa haraka kwa abiria wote ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza, kwani matumizi ya kadi hizo ni rafiki na njia rahisi ya kulipa nauli.
Amefafanua kuwa miongoni mwa faida za matumizi ya kadi janja ni pamoja na kuzuia udanganyifu na kuongeza mapato, huku akiwataka kuongeza idadi ya mabasi ili usafiri huo uleta tija kama ulivyokusudiwa.
katika hatua nyengine Mhe. Mchengerwa ametoa maagizo kwa DART kwa kushirikiana na Kampuni ya Kutoa Huduma ya Mabasi (UDART) kuhakikisha wanaongeza idadi ya magari na hadi kufikia mwezi Disemba mwaka huu usafiri wa mabasi Yaendayo haraka uwe umeanza katika barabara ya Mbagala.
“Naomba muwakaribishe wazabuni ambao watashirikiana na serikali kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka na kuleta ufanisi katika utekeleza wake” amesema Mhe. Mchengerwa.
Mtendaji Mkuu Wakala wa Mabasi ya Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Athuman Kihamia, amesema kuwa mfumo wa matumizi ya kadi janja ni rafiki kwa abiria kwani ni mradi ambao unasaidia utunzaji wa mazingira.
“Mfumo huu uliojengwa na Wataalam wa Mabasi Yaendayo Haraka una faida nyingi ikiwemo kuondoa uchafuzi wa mazingira, zitasaidia kuondoa usumbufu wa chenji pia kuondoa foleni za kununua tiketi, pia kadi hizi zina ubora ukilinganisha na nyingine zinazotumika huko” amesema Dkt. Kihamia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa DART, Dkt. Florens Turuka, amesema kwa DART ni jambo la fahari kuona mifumo inaimarika kwenye kuendesha usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka na dhamira yao ni kuona kuwa mifumo hii inarahisisha na kuleta tija Jiji la Da es Salaam.
Kadi na Mageti janja yaliyozinduliwa yanayotokana na Mfumo wa Serikali wa Ukusanyaji nauli (AFCS) ni juhudi za serikali katika kutumia wataalam wa ndani kuunda mifumo itakayotoa suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika kuzifikia huduma na kuleta tija kwa Taifa.