Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakagwe, Kata ya Butobela, Wilaya ya Geita, Daudi Lumala, amekanusha vikali taarifa zinazodai kuwa wachimbaji wadogo katika machimbo yasiyo rasmi (rash) eneo la Mabunduki wanadhulumiwa na matajiri.
Lumala, akizungumza na waandishi wa habari, ameeleza kuwa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo zinaendelea kwa amani na hakuna malalamiko yoyote yaliyotolewa kuhusu wizi au udhulumu wa dhahabu wakati wa kugawana mapato yanayozalishwa. Amesisitiza kuwa habari zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan kwenye makundi ya WhatsApp, ni za uongo na uzushi, akibainisha kuwa hakuna mtu yeyote aliyedhulumiwa katika uzalishaji uliofanyika machimboni hapo.
“Taarifa zinazodai kwamba kuna udhulumu wa dhahabu hapa Mabunduki ni za uongo. Uchimbaji unaendelea kwa utulivu na haki,” alisema Lumala.
Katika uzalishaji wa hivi karibuni katika eneo hilo, Lumala alisema jumla ya shilingi milioni 63 zimekusanywa, fedha ambazo zitatumika kujenga jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Nyakagwe, ambapo kwa sasa walimu wanatumia darasa kama ofisi.
Meneja wa machimbo ya Mabunduki, Mgusa Sylvester, ameunga mkono kauli ya mwenyekiti huyo, akieleza kuwa mapato yaliyopatikana yamegawanywa bila malalamiko yoyote. Ameongeza kuwa kodi za serikali zimelipwa na mchango wa maendeleo kijijini umetolewa, alibainisha Sylvester.
Habari hizi zinakuja baada ya madai yasiyo na msingi kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo limezua taharuki miongoni mwa wachimbaji na wakazi wa eneo hilo.