Na Prisca Libaga Maelezo Arusha
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, Septemba 02, 2024 anatarajiwa kufungua Jukwaa la 24 na Mkutano wa 35 wa kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, (UNFCCC, standing Commitee on Finance).
Taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, ofisi ya Makamu wa Rais imesema kuwa Mkutano huo utakaoanza Septemba 2 na kumalizika Septemba 6, utafanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Taarifa hiyo imesema kuwa Mkutano huo ambao ni mara ya kwanza kufanyika nchini, ni maandalizi ya Mkutano wa COP29 unaotarajiwa kufanyika Novemba 11-22, 2024 mjini Baku, nchini Azerbaijan.
Taarifa imesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo nchini, kunatokana na ombi la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliomba (United Nations Framework Convention on climate change)…. andika kwa kiswahili chake (UNFCCC) kuruhusu kamati yake ya fedha kuja kufanya mkutano huo muhimu hapa nchini.
Taarifa imesema kuwa Mkutano huo ambao utahudhuriwa na washiriki 200 kutoka nchi zaidi ya 80 utawezesha upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Taarifa hiyo imesema kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Kuongeza Kasi Katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Ufadhili Unaozingatia Jinsia”.
Kamati ya kudumu ya fedha ni moja ya kamati chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi iliyoundwa katika mkutano wake wa 16 wa Nchi Wanachama (COP16).
Lengo la kamati hiyo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa shughuli za mkataba na Kamati hiyo ambayo ina jumla ya wajumbe 32 waliochaguliwa kutoka nchi zinazoendelea na zilizoendelea ambazo ni wanachama wa mkataba huo.