Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Mkoa wa Geita (GRWFA) kimefanya uchaguzi wa viongozi wapya ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Uchaguzi huo umefanyika katika ofisi za chama hicho, chini ya usimamizi wa Wakili Mark Chota.
Katika uchaguzi huo, Elizaberth Makwenda amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa GRWFA baada ya kupata kura 3, huku mpinzani wake, Veronica Samo, ambaye alikuwa akitetea kiti hicho, akipata kura 1 pekee. Matokeo hayo yalitangazwa na msimamizi wa uchaguzi, Wakili Mark Chota, mbele ya wajumbe wanne ambao walipiga kura.
“Nataka kutangaza kwamba Elizaberth Makwenda ndiye mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Geita kwa kura 3 dhidi ya 1 aliyopata Veronica Samo.” Alisema Mark Chota – Msimamizi wa Uchaguzi
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita, Salum Kulunge, aliwataka viongozi wapya kuwa wamoja na kuvunja makundi yote yaliyokuwepo wakati wa kampeni ili kuleta mshikamano na maendeleo katika soka la wanawake mkoani humo.
“Ninawasihi viongozi wapya kushirikiana kwa pamoja ili kuendeleza soka la wanawake. Lazima tuhakikishe tunavunja makundi na kufanya kazi kwa umoja.” Alisema Salum Kulunge – Mwenyekiti wa GeREFA Mkoa wa Geita
Elizaberth Makwenda, Mwenyekiti mpya, ameahidi kuboresha na kusukuma mbele soka la wanawake katika mkoa huo, akiahidi kuwa na mikakati thabiti kwa maendeleo ya mchezo huo. Naye Veronica Samo, aliyemaliza muda wake, ameahidi kushirikiana na Mwenyekiti mpya kwa maslahi ya soka la wanawake.
“Nitaweka mikakati madhubuti kuhakikisha soka la wanawake linaendelea kukua na kupata mafanikio makubwa zaidi katika mkoa wetu.” Elizaberth Makwenda – Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Geita
Uchaguzi huu umefanyika kwa mujibu wa kanuni, ambapo wapiga kura walikuwa ni wenyeviti wa vilabu vya wanawake vilivyosajiliwa rasmi na TFF katika Mkoa wa Geita.