Na John Walter -Babati
Naibu waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa Daniel Sillo amesema Serikali itaendelea kuwachukulia hatua madereva wazembe wasiotii na wanaokiuka Sheria za usalama barabarani.
Ameyasema hayo leo mkoani Manyara alipofika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya gari iliyotokea asubuhi ya leo Agosti 31, 2024 Kijiji cha Gajal wilaya ya Babati na kusababisha vifo vya Wanafunzi watatu wa shule ya Sekondari Endasaki na dereva aliyekuwa anaendesha gari lililokuwa limebeba Wanafunzi wakielekea mkoani Arusha.
Kwenye ajali hiyo Watu wanne wamefariki dunia na wengine 30 wamejeruhiwa baada ya gari aina ya Costa yenye namba za usajili T 187 DXV kugongana na gari la mizigo Scania lenye tela namba RL 5485 katika Kijiji cha Gajal wilaya ya Babati mkoa wa Manyara.
Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara kamishna msaidizi mwandamizi Makarani Ahmed akizungumza katika eneo la tukio, amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari hilo aina ya Scania aliyehama upande wake bila kuchukua tahadahari.
Makarani amesema majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara kwa matibabu huku Watano wakiwa katika hali mbaya (ICU).
Kamanda amewataka madareva na watumia barabara kwa ujumla kuwa waangalifu pindi wanapoendesha ili kuepuka ajali zinazosaabisha vifo vya watu na ulemavu wa kudumu.
Hata hivyo Kamanda amesema dereva huyo raia wa Burundi baada ya kusababisha ajali alikimbia na jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Naye diwani wa kata ya Dareda Sabini John amesema eneo hilo la Gajal lenye mlima na mteremko mkali lina historia ya ajali za mara kwa Mara.