Mabalozi wamehimizwa kuzishawishi kampuni zenye mitaji, teknolojia na dhamira ya dhati kuja kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ambayo hayajatumika ipasavyo nchini Tanzania kutokana na sababu mbalimbali ambazo ni pamoja na ukosefu wa mitaji, teknolojia na miundombinu wezeshi.
Hayo yamejiri wakati wa vikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo (Mb) na Mabalozi wa nchi mbalimbali aliokutana nao kwa nyakati tofauti jijini Dar Es Salaam Agosti 30, 2024 kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi hizo pamoja na kujitambulisha.
Mabalozi hao ni Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Marekhi; Balozi wa Kuwait, Mhe. Mubaraka Mohammed Alsehaijan; Balozi wa Brazil, Mhe. Gustavo Martins Nogueira na Balozi wa Ubelgiji, Mhe. Peter Huyghebaert.
Waziri Kombo alisifu uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na nchi hizo na kuwaomba Mabalozi hao kufikisha salamu za shukrani za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Wakuu wa nchi zao ambao muda wote wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo ya Tanzania.
Balozi Kombo alisema nchi hizo zimekuwa zikiipatia Tanzania misaada mbalimbali ya mendeleo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha Tanzania hapa ilipofika sasa.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuisadia Tanzania pamoja na kuimarisha mifumo ya kushirikiana katika bisahara na uwekezaji kwa kuzitaka nchi hizo kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, madini, nishati, ujenzi wa viwanda vya madawa, utalii na elimu ya ufundi.
Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu wezeshi kama usafiri wa moja kwa moja wa ndege baina ya Tanzania na nchi hizo na kutunga sera, sheria na kanuni zitakazohamasisha biashara na uwekezaji, na kuondoa vikwazo vyote vinavyozorotesha uwekezaji
Aliahidi yeye na timu yake Wizarani itasimamia ukamilishwaji wa Hati za Makubaliano pamoja na mikataba ya Utozaji wa Kodi Mara mbili na ya Kulinda Vitega Uchumi ambayo imekuwa ikihitajika na kampuni nyingi zinazotaka kuwekeza nchini.
Waziri Kombo alimalizia kwa kusisitiza umuhimu wa mawasiliano kama njia muhimu ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Tanzania na nchi hizo pamoja na muingiliano wa watu wa ngazi zote, iwe Wakuu wa Nchi, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na sekta binafsi.