Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa siku 14 mbele ili kutoa fursa kwa waombaji wa mikopo waweze kutimiza azma yao ya kuomba mikopo.
Ongezeko la siku 14 linafanya sasa zoezi la uombaji kufikia tamati Septemba 14 mwaka huu kwani awali zoezi hili lilipaswa kufungwa Agosti 31. Uamuzi wa kuongeza siku 14 zaidi unatokana na baadhi ya waombaji kushindwa kukamilisha maombi yao, hivyo waombaji wote ambao hawajakamilisha zoezi la uombaji mikopo wanapaswa kutumia siku zilizoongezwa kukamilisha maombi yao ili waweze kunufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Akisisitiza kuhusiana na muda ulioongezwa, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema “Tumeona kuna sababu za msingi za kuongeza muda wa wiki mbili ambazo zinatoa muda wa kutosha kuwapa nafasi wale ambao hawajaomba kuweza kuomba ili kila muhitaji wa mkopo aweze kupata nafasi ya kuomba mkopo.”
Ikumbukwe kuwa hii ni fursa ya mwisho iliyotolewa na HESLB kwani hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza kwa waombaji watakaoshindwa kuwasilisha maombi yao ifikapo Septemba 14.