Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt Festo Dugange amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Susuni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ili kuwasogezea karibu huduma za afya Wananchi wa kata hiyo.
Mhe. Dkt. Dugange amesema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma, katika kipindi cha Maswali na Majibu, wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara aliyeuliza Je, Ni lini Serikali itajenga kituo cha afya Kata ya Susuni Jimbo la Tarime Vijijini?
Mhe. Dkt Dugange amesema Kata ya Susuni iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ina jumla ya Vijiji vitano (5) vya Matamankwe, Kiongera, Keroti, Kikomili na Nyabilongo. Kati ya vijiji hivyo, Vijiji viwili (2) vya Matamankwe na Kiongera vina zahanati, Kata haina Kituo cha Afya.
Amesema Serikali imepanga kuipandisha hadhi Zahanati ya Kiongera kuwa kituo cha afya ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepeleka fedha shilingi Milioni 207 kwenye Zahanati ya Kiongera kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wazazi lenye huduma ya upasuaji wa dharura na jengo la Maabara”.
Sanjali na hayo Dkt. Dugange amesema Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti mbalimbali zitakazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini ili kukamilisha mradi huo wa ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Susuni.
“Katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri itatenga shilingi Milioni 150 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu iliyosalia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la kufulia, jengo la kuhudumia Wagonjwa wa nje (OPD) na jengo la Wodi ya kulaza Wagonjwa.” Dkt Dugange.