Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ameipongeza Benki ya Biashara Tanzania kufuatia uthubutu wake kwa kuunga mkono juhudi za wadau wa Sanaa katika kuendeleza Sekta hiyo.
Katibu Mkuu ametoa pongezi hizo tarehe 29 Agosti, 2024 Jijini Dar Es Salaam wakati akizindua Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya Filamu na Sanaa Tanzania ambapo Benki hiyo itakuwa mdhamini Mkuu wa Tamasha hilo.
“Naipongeza sana Benki ya Taifa ya Biashara kwa kuamini katika Sekta ya Sanaa na kuweka fedha kufanikisha Tamasha hili” amesema Ndugu Msigwa.
Aidha, Tamasha hilo litafanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 11 – 15 Disemba, 2024 ambapo litaratibiwa na Taasisi yake kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania.
Lengo kuu la Tamasha ni kuwakutanisha wadau wa Filamu, Sanaa, pamoja na wadau wa Sekta mtambuka katika jukwaa moja ili kujadili mustakabali wa Maendeleo hususan katika masoko, teknolojia na ushirikiano wa kitaifa na kimataifa ili kukuza na kuendeleza Masoko ya kazi za Filamu na sanaa kwa ujumla.
Ndugu Msigwa ametoa rai kwa Taasisi zingine za kifedha kuungana na TCB kushirikiana na wadau wa Sanaa nchini katika kutengeneza kazi nzuri za Sanaa kwakuwa Sanaa ni moja ya Sekta kubwa zinazolipa na kurudisha faida kama uwekezaji ukifanyika vizuri ambapo hadi sasa Sekta hiyo inaongoza kwa ukuaji kwenye uchumi nchini kwa asilimia 17.
Katika hatua nyingine Gerson Msigwa amewataka wadau wa Filamu kufungamana na Tasnia zingine ikiwemo utalii, biashara, uwekezaji pamoja na huduma za jamii ili kuongeza wigo wa biashara, ambapo ameielekeza Bodi ya Filamu kuitisha mjadala wa pamoja kati ya wasanii na wadau wengine kujadili fursa zilizopo kwenye Sekta zao.
Ameongeza kuwa Wasanii nchini wanatakiwa kujiendeleza kielimu ili wakuze maarifa katika kufanya kazi zao na kufikia viwango vya kimataifa tofauti na kutegemea vipaji pekee bila kuwa na taaluma sahihi ya Sanaa wanazozifanya.
Pamoja na mambo mengine amewataka Wasanii nchini kuacha migogoro na kuungana katika kufanya kazi kwasababu migogoro inarudisha nyuma Sanaa zao na kukwamisha maendeleo, vilevile Serikali haipendi kujihusisha na jamii au Taasisi zenye migogoro.