VICTOR MASANGU, KIBAHA
Diwani wa kata ya Visiga katika Halmashauri ya mji Kibaha Mhe. Kambi Legeza katika kuunga mkono na kuchagiza chachu ya maendeleo katika sekta ya elimu ameamua kutoa msaada wa mtambo maalumu wa kusaidia kutolea nakala mbali mbali za karatasi ‘Photocopy mashine’ katika shule ya msingi visiga kwa ajili ya kuwasaidia walimu na wanafunzi kuondokana na adha waliyokuwa nayo.
Kambi ametoa msaada wa mashine hiyo wakati sherehe ya mahafali ya shule ya msingi Visiga ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kuweza kuwaaga wanafunzi waliomaliza wa darasa la saba wapatao 248 ambao wamefanikiwa kuhitimu katika hatua hiyo ngazi ya msingi na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali, wakiwemo wa chama, wazazi , walimu, walezi pamoja na wazazi.
Kambi amesema kwamba amesema kwamba ameamua kutoa msaada huo kutokana na kubaini katika shule hiyo kuna uhitaji mkumbwa kupeleka mashine hiyo ambayo itakuwa ni mkombozi mkubwa katika kuwasaidia walimu na wanafunzi ambao wamekuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kutumia gharama kubwa hivyo itaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa upande wao.
“Mimi kama Diwani wa kata ya Visiga nimebaini kuna changamoto kubwa na wazazi na walezi kuchanga michango mbali mbali kwa ajili ya kutoa nakala za mitihani hivyo kunatumika gharama nyingi sana kwa hivyo nikaona kuna umuhimu mkubwa kupitia mahafali haya niweze kutoa mashine hii ya Photocopy ambayo nina amini itaweza kuleta mageuzi makubwa katika shule hii ya msingi Visiga,”alisema Mhe. Kambi
Pia aliongeza kwamba lengo lake kubwa ni kuweza kuweka mikakati kabambe kwa ajili ya kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo hivyo ameahidi kuendelea kutoa sapoti katika shule nyingine zilizobaki ili kuweza kukuza na kuboresha sekta ya elimu kwa ngazi ya msingi na Sekondari katika Kata ya Visiga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Visiga Kasmir Komba amempongeza kwa dhati Diwani huyo kwa kuweza kutoa mashine hiyo ambayo itaweza kwenda kupunguza changamoto ya siku nyingi ambayo ilikuwa inawakabili katika suala zima la kutoa nakala mbali mbali hasa katika kipindi cha kutolea mitihani na mambo mengine ya muhimu.
Mwenyekiti huyo aliongeza kwamba shule hiyo ambayo imeaanzishwa mnamo mwaka 1992 imekuwa ikifanya vizuri kwa wanafunzi wake katika mitihani mbali mbali japo inakabiliwa na baadhi ya changamoto mbali mbali zikiwemo uhaba wa madawati, pamoja na uchakavu wa madirisha kwa baadhi ya madarasa.
Nao baadhi ya wazazi ambo wamehudhuria katika mafali hayo akiwemo Zainabu Abdalah hawakusita kutoa pongezi zai za dhati kwa Diwani wa kata ya Visiga ambaye ameweza kuondoa kero ya michango mbali mbali ambayo walikuwa wakichangishwa na walimu kwa ajili ya kutoa nakala za mitihani hivyo mashine hiyo itawaondolea kabisa baadhi ya michango.
Alifafanua kwamba kabla ya kutolewa kwa mashine hiyo hapo awali wazazi na walezi walikuwa wanachangia kiais cha shilingi elfu 1200 ili mtoto aweze kupata huduma ya kufanya mitihani jambo amabalo lilikuwa ni usumbufu mkubwa kutokana na hali ya kipato na uchumi waliyonayo lakini kwa kitendo alichokifanya diwani huyo kinafaa kuigwa kwa viongozi wengine.