Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita (watatu kutoka kushoto), akipokea vifaa tiba kutoka kwa Stanley Kafu, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim ukiwa ni mchango wa benki hiyo katika jitihada za kuboresha huduma za afya katika makabidhiano ambayo yamefanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga mnamo tarehe 29 Agosti, 2024.
………………
Shinyanga: Benki ya Exim Tanzania imetoa msaada wa vifaa tiba ya afya kama sehemu ya mchango wake katika jitihada za kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Makabidhiano hayo ambayo yamefanyika mbele ya Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, yanalenga kusaidia kupunguza changamoto za huduma za afya katika wilaya hiyo katika tukio ambalo limefanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama mnamo tarehe 29 Agosti, 2024.
“Takwimu zinaonesha kama taifa tumepiga hatua katika kuongeza na kuboresha miundominu katika vituo vya afya nchini, lakini changamoto ya vifaa tiba pamoja na wataalamu wa afya bado ipo. Utoaji huu wa vifaa tiba ni sehemu ya mpango wetu mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini,” anasema Stanley Kafu, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania.
Kupitia mpango wa ujulikanao kama ‘Exim Cares’, benki ya Exim imekuwa ikichangia katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika sekta za elimu, mazingira, utalii, Uchumi, na afya. Hii ni sehemu ya dhamira yake ya kuboresha maisha ya kila Mtanzania popote alipo nchini.
Kafu anaongeza kuwa, “Tumekuwa tukishiriki katika mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya. Mfano mwaka huu, tumeshiriki katika kampeni ya kitaifa ya uchangiaji damu katika mikoa mbalimbali, vilevile tumetoa vitanda vya kujifungulia wajawazito Mkoani Morogoro pamoja na vitanda vya hospitali Mkoani Tanga na kufanikiwa kumaliza tatizo la uhaba wa vitanda katika kituo cha afya, Mwakadila.”
Benki ya Exim Tanzania ni moja kati ya benki kubwa tano hapa nchini yenye matawi yake katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini Tanzania. Benki hiyo pia inajivunia kuwa benki ya kwanza ya Kitanzania kuvuka mipaka na mpaka sasa wanapatikana katika nchi za Djibouti, Comoro, na Uganda.