Na Neema Mtuka, Rukwa
Wananchi mkoani Rukwa wametakiwa kuachana na vitendo vya rushwa na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona na kusikia kuhusu vitendo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Rukwa Mzalendo Widege amesema kuwa jukumu la kuzuia rushwa ni la kila mwananchi.
Mzalendo amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2024 TAKUKURU Mkoa wa Rukwa imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kupitia madawati ya kuzuia rushwa ,elimu kwa umma pamoja na uchunguzi wa mashtaka.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho wamesimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi nane ya maendeleo yenye thamani ya sh 784,200,000 ili kujua kama kweli fedha iliyotumika imefanya kazi kama ipasavyo na kubaini kasoro ndogo na tayari hatua stahiki zimechukuliwa ili kukabiliana na kasoro hizo.
Aidha amesema kuwa wanaendelea na uchambuzi wa mifumo mbalimbali hasa ya utoaji wa huduma kwa wananchi lengo likiwa ni kubaini mianya ya rushwa na kisha kuweka njia ya kuiziba .
Amesema lengo hasa ni kuhakikisha kila mwananchi wa rika na kada mbalimbali katika mkoa wa rukwa na wanaendelea kutoa elimu na uelewa juu ya vitendo vya rushwa .
Hali kadhalika Mzalendo amesema kuwa ni muhimu wananchi wakashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa ndani ya jamii .
Pia wameendelea na kazi ya uelimishaji umma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo katika kipindi hiki zimefanyika semina 24 katika halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ,sumbawanga vijijini na wilaya za Kalambo na Nkasi.
Mzalendo amesema wamepokea taarifa 62 kati ya hizo taarifa 49 zilihusu rushwa ambapo ofisi inaendelea kuzifanyia kazi na uchunguzi wake unaendela katika hatua mbalimbali.
Ambapo taarifa hizo 13 kati ya 62 zilizopokelewa hazikuhusu rushwa hivyo ofisi hiyo imetoa ushauri kwa watoa taarifa na kuwaelekeza mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko hayo na hakukuwa na taarifa iliyohamishiwa idara nyingine.