Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Florian Kabaka ameitaka Wakala hiyo kuhakikisha inaendelea kuwajengea uelewa wananchi kuhusu majukumu ya TARURA ikiwemo utafiti na udhibiti ubora wa vifaa vya ujenzi unaofanyika kupitia maabara za Wakala huo.
Mhandisi Kabaka ameyasema hayo leo Agosti 28,2024 alipotembelea banda la maonesho la TARURA kwenye kikao kazi cha Wenyeviti na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kinachofanyika kwenye ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Amesema utoaji wa elimu utasaidia kujenga mahusiano na wananchi na kuelewa kazi kubwa inayofanywa na TARURA katika matengenezo na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
“Nawapongeza kwa ushiriki huu lakini hakikisheni mnaendelea kushiriki kwenye maonesho mengine kama haya ili kuwaeleza wananchi kazi nzuri tunazozifanya na kujibu hoja zao mbalimbali ”.