NA MWANDISHI WETU, KAGERA.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera Jumatatu Agosti 26, 2024 imetoa hukumu dhidi ya Mjasiriamali INNOCENT RWEKAZA BANYEZA na mwenzie Bw. JASPER JOSEPHAT BALOZI ambaye ni Karani wa Kampuni ya Kahawa TANICA PLC.
Mahakama hiyo imemtia hatiani Bw. INNOCENT R. BANYEZA kwa makosa matatu ya kuwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu kutoka SIDO kinyume na k/f cha 302 na 342 katika Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Hukumu hiyo dhidi ya Bw. BANYEZA imetolewa katika Kesi ya Jinai Na. 38/2023 mbele ya Mhe. Wilson Yona SRM Hakimu Mkazi Mwandamizi – Mahakama ya Hakimu Mkazi Kagera.
Shauri hili limeendeshwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Bw. William Fussi.
Mshtakiwa wa kwanza amepewa adhabu ya kulipa fine ya sh. 50,000 au kwenda jela mwaka mmoja kwa kila kosa la kutumia nyaraka za uongo na kupewa adhabu ya kifungo cha nje miezi sita kwa kosa la kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu. Vilevile,
ameamriwa na mahakama kurejesha kiasi cha sh. 2,500,000 alichokipata SIDO kwa udanganyifu.
Mshtakiwa wa pili yeye ameachiwa huru kwa kuwa taarifa ya kitaalamu ya maandishi haikuweka bayana ni nani aliyeghushi.