Na WAF – Brazzaville, Congo
Rais wa Congo Brazzaville, Mhe. Denis Sassou Ng’uesso amesisitiza umuhimu wa kuendelea na mikakati ya kuzuia magonjwa ya milipuko kwa kutumia chanjo kwa kuwa magonjwa hayo hutokea wakati wowote.
Rais Ng’uesso amesema hayo leo Agosti 26, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Afya wa 74 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika uliowakutanisha Mawaziri kutoka katika nchi hizo.
“Nchi wanachama bado inakabiliana na magonjwa, majanga na matukio mbalimbali ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja, tuendelee kuweka mikakati ya Afya ya Msingi ili kukabiliana na majanga haya.” Amesema Rais Ng’uesso
Amesema, magonjwa hayo mengi ya mlipuko yanatokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja kwa usalama wa mazingira yetu na usalama wa binadamu kwa ujumla.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Tanzania Mhe. Jenista Mhagama wakati akichangia mada katika mkutano huo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini usaidizi wa WHO katika kupambana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Amesema, pamoja na maandalizi ya dharura, Serikali ya Tanzania inatoa shukrani za dhati kwa ‘Regional Director’ na WHO ambapo kwa pamoja inawezekana kujenga Afrika yenye ustahimilivu zaidi.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunampongeza Mkurugenzi kwa uongozi na kuipongeza kwa kuongoza vizuri Afrika katika ‘International Health Regulations’ (IHR) na tunatazamia kukamilishwa kwa mkataba wa janga hili.” Amesema Waziri Mhagama
Nae, Waziri wa Afya Congo Brazzaville, Mhe. Gilbert Mokoki amesisitiza nchi wanachama kuweka kipaumbele cha fedha za kusaidia Shirika la Afya Duniani kupitia Programu ya 14 ya Shirika hilo.
“Tuweke mikakati ya pamoja ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa MPOX ili kuwa na Afya kwa wote.” Amesema Waziri Mokoki