Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe akizungumza na waandishi wa habari.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe akisisitiza jambo katika mkutano huo kulia ni Mwandishi Esther Christopher kutoka chama cha wahadisi wanawake na kushoto ni mwalimu Ndabazi mnufaika wa mpango wa STEM.
…………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolf Mkenda anatarajiwa kufungua Mbio za ERB STEM Marathon 2024 ambazo zitashirikisha Jumuiya ya Wahandisi pamoja na wadau mbalimbali kwa ajili ya kutafuta shilingi bilioni mbili zitakazo kwenda kusaidia Shule zenye upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi nchini.
Akizungumza Agosti 26, 2024 katika Ofisi ndogo za Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Jengo la PSSSF Barabara Sam Nujoma Mlimani Ciy jijini Dar es Salaam kuhusu Kongamano la Wahandisi na Mbio za ERB STEM Marathon 2024, Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe, amesema kuwa mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Septemba 7, 2024 maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mhandisi Kavishe amesema kuwa wahandisi wameanzisha mradi wa Stem Supports Pragram wenye lengo la kuwafadhili walimu wenye shahada kwenda kufundisha katika shule zenye uhitaji nchini.
“Nawakaribisha watu wote kushiriki kwa ajili ya kujenga afya na ambao hawana uwezo wa kukimbia wanaweza kuwadhamini wakimbiaji au kununua vifurushi vya walimu” amesema Mhandisi Kavishe.
Mhandisi Kavishe amesema kuwa fedha zitakazopatikana zinakwenda kuwalipa walimu posho ya kila mwezi, nauli pamoja na bima, huku akibainisha kuwa kila mwalimu mmoja atatumia gharama ya Sh. 900,000.
“Sisi tutawafadhili kwa muda wa miaka miwili na shule husika itatoa mahali pa kulala, chakula pamoja na kuwakuza kitaalamu” amesema Mhandisi Kavishe.
Mhandisi Kavishe amesema kuwa pia Septemba 3 hadi 4, 2024 kutakuwa Kongamano la wahandisi vijana litakalofanyika PSSSF Comerce Complex ambalo limelenga kuwapa mafunzo ya biashara ikiwemo namna ya kuanzisha kampuni.
“Watapewa miradi miwili au mitatu kwa ajili ya kushikwa mikono baada ya hapo watakuwa na mpango ambao watawasidia katika kufikia malengo yao” amesema Mhandisi Kavishe.
Mhandisi Kavishe amefafanua kuwa Septemba 5 hadi 6, 2024 kutakuwa na mkutano wa wahandisi ambao utafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City.
Amesema kuwa katika mkutano huo wahandisi watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kuonesha maonesha ya kazi zao pamoja na kula viapo kwa wahandisi wapya.