Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Dodoma.
Ni sahihi kabisa kusema kwamba hakuna mwanadamu aliyekamilika, iwe kitabia na kimahitaji. Kwamba huyo ana tabia zote nzuri asilimia 100. Vilevile hakuna anayeweza kujitosheleza mwenyewe kimahitaji bila msaada wa binadamu wenzake. Hata mtu awe bilionea namba moja duniani, anawahitaji watu wengine wa ngazi za chini kuweza kumkamilisha kimahitaji na kimafanikio. Hata mlinzi wake nyumbani anaweza kuwa hitaji muhimu sana kwake mbali na daktari wake, mwanasheria wake, mshauri wake na wengine. Kiufupi tunahitajiana na hivyo hata mtumishi wa ndani au mlinzi, usimadharau. Ni hitaji muhimu. Ngoja tuone mifano minne katika dhana hii ili unielewe vizuri ndugu msomaji wangu.
Mosi, gari la tajiri likipata pancha, anaenda kuliziba kwa watu wa kawaida kabisa kwa sababu hawezi kuziba pancha mwenyewe. Pili, tajiri anayemiliki viwanda, wafanyakazi wake ni watu wa kawaida ambao kupitia nguvu na akili zao wanamwongezea uzalishaji viwandani na hivyo anaendelea kuwa tajiri kupitia maendeleo ya viwanda yatokanayo na jasho la wafanyakazi wake wa chini. Tatu, tajiri au tuseme mfanyabiashara anayemiliki kiwanda vya kuzalisha unga wa ngano, wateja wake ni watu wa kawaida kabisa kama vile mamalishe na babalishe wanaouza maandazi na chapati. Wanaponunua unga wa kukandia maandazi na chapati zao, ndipo tajiri anayemiliki kiwanda cha unga wa ngano anavyozidi kuwa bilionea. Hawa wakikosekana kiwanda kinakufa.
Nne, mwanasiasa, mathalani mbunge, ukifika wakati wa uchaguzi na kulazimika kuzunguka kuomba kura kwa wananchi, hata awe na makeke kiasi gani lakini atalazimika kuwa mpole, atajishusha, atacheza na wananchi wenzake ngoma za asili na wakati mwingine hadi kupiga magoti akiomba kura kwa wananchi maskini kwani anajua ni wao pekee kumfanya aitwe mbunge na si vinginevyo.
Hivyo, tunategemeana katika haya maisha ndugu yangu. Acha kupandisha mabega ukidhani wewe ni bora kuliko wengine kwa sababu ya pesa, kutoka ukoo bora, madaraka ulio nayo au chochote kile. Kimsingi huwezi kusimama, kuendelea na kupiga hatua za maendeleo bila mchango wa watu wengine. Nimeanza na utangulizi na mifano hiyo ili kuunga mkono kampeni ya ‘Tutunzane Mvomero” Hii ni kampeni yenye kaulimbiu; _“Mfugaji Mtunze Mkulima na Mkulima Mtunze Mfugaji ili Kulinda Mazingira Yetu.”_ Ni kampeni inayosimamiwa kikamilifu na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli ambayo ilizinduliwa Agosti 3, 2024 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Morogoro.
Kimsingi, kampeni hii ni muhimu katika jitihada za kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo kupitia utoaji wa elimu kwa makundi haya mawili ili kuondoa uadui dhidi yao kwani kila mmoja anamtegemea mwenzie katika maisha yake. Mvomero ni sehemu ndogo ya Tanzania yetu ambayo imekuwa ikikumbwa na migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji. Yapo maeneo mengi yenye migogoro ya ardhi inayosababisha magomvi baina ya wakulima na wafugaji na pengine kuhatarisha maisha. Hivyo kampeni ya Tutunzane inapaswa kuvuka mipaka ya Mvomero na kwenda nchi nzima ili kuhakikisha amani inakuwepo kwa kumaliza ugomvi kati ya wakulima na wafugaji na kuchangia maendeleo kwani sekta hizi mbili; kilimo na ufugaji ni muhimu sana katika maendeleo.
Wakulima na wafugaji wanategemeana. Kwa mfano, mfugaji hawezi kuishi kwa kutegemea kula mazao ya mifugo yake pekee kama vile nyama na maziwa, vilevile mkulima hawezi kuishi kwa kutegemea kula mazao kutoka shambani kwake tu, kwani kuna wakati anahitaji kula nyama na kunywa maziwa kutoka kwa mfugaji ili aweze kujenga afya bora kupitia mlo kamili kama tunavyoshauriwa na wataalamu wa afya na lishe.
Lakini hata katika maisha ya kawaida, wakulima na wafugaji wanapaswa kuishi kwa amani kwani kwa miaka mingi, makundi haya mawili wamekuwa ni ndugu wanaoishi pamoja, wanaosali katika nyuma za ibada pamoja, watoto wao wakisoma shule moja na kufanya mambo mengi pamoja ya karaha na furaha kama vifo, misiba na harusi. Hakuna aliye bora zaidi ya mwenzake, wanahitajiana na wanategemeana pia. Kutokana na ukweli kuwa ardhi ni nyenzo muhimu ya maendeleo, ni lazima ardhi ya kijiji ipimwe na kujua mipaka na kisha kuwa na matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara inayohatarisha amani na ustawi wa maendeleo.
Ni muhimu vijiji kutenga eneo kwa ajili ya malisho, eneo kwa ajili ya mashamba, eneo la msitu wa kijiji, eneo la makazi, eneo la miradi ya kijamii na maendeleo kama shule, soko, kituo cha afya, ofisi mbalimbali, viwanda na kadhalika. Kupitia sheria ndogo za kijiji (by-laws) zingeeleza adhabu hususani za faini kwa mtu anayekiuka matumizi bora ya ardhi ikiwemo kulisha mashamba, kukata miti kwenye msitu bila kibali, kuharibu vyanzo vya maji na kadhalika.
Kampeni ya Tutunzane imelenga kuhamasisha wakulima na wafugaji kurasimisha ardhi zao kwa gharama nafuu ili waweze kupata hati miliki za mashamba yao ili wapewe mbegu za malisho na ufuta kwa ajili ya kupanda. Katika ardhi zao zilizopimwa, wafugaji watakuwa na uwezo wa kupanda malisho mazuri kwa ajili ya chakula cha mifugo yao na kuepukana na kadhia ya kwenda kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima ambapo inaleta ugomvi, uhasama na kuwatia hasara wakulima kwa kupoteza mazao yao na hivyo kuendelea kuishi maisha duni.
Kampeni inasisitiza ufugaji wa kisasa ikiwemo kuwa na maeneo yao ya kulima malisho ili kuondokana na migogoro kati yao na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi. _“Kampeni hii ni muhimu kwa sababu inakwenda kuleta amani, kuleta ongezeko la malisho, tija na wafugaji waweze kukopesheka”_ anasema Rais Samia katika uzinduzi wa kampeni hiyo.
Aidha, kampeni hii pia inachochea maendeleo kwa kuweka mkazo wa kuwa na eneo dogo lakini lenye uzalishaji mkubwa kwa kufuata mbinu za kisasa za uzalishaji kwani utaalamu unaonesha kuwa ili kuwa na tija kubwa kwenye kilimo, hakuna haja ya kulima eneo kubwa au ili kuzalisha nyama na maziwa mengi si lazima kuwa na mifugo mingi, bali ni kufuata mbinu za kisasa. Kwa mfano, huwa inaelezwa kwamba kufunga ng’ombea watatu, uzito wa kilo zake na maziwa wanayotoa ni sawa na ng’ombe mmoja aina ya Boran ambayo ni ng’ombe wa kienyeji walioboreshwa. _“Lazima tuwe wabunifu wa kuja na mbinu zitakazofanya ardhi tuliyonayo izalishe zaidi. Kama ni mkulima azalishe zaidi kwa kipande cha ardhi alichonacho, vivyo hivyo kwa mfugaji,”_ anasema Rais Samia.
_*TUTUNZANE NA 4R ZA RAIS SAMIA*_
Rais Samia anaongoza nchi kwa kutumia falsafa yake ya R nne, yaani _Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya)._ Kutokana na uwepo wa uhasama kati ya wakulima na wafugaji, kuna haja kubwa ya kuwa na maridhiano baina yao kwa kuweka mikakati madhubuti ikiwemo Kampeni ya Tutunzane ili kuleta amani na ndio maana ninasisitiza kwamba hii inapaswa kuwa kampeni ya kitaifa. Kumbuka ni kampeni pia inayosisitiza umuhimu wa kuleta mabadiliko kwa kulima na kufuga kisasa.
Vilevile, kampeni hii inalenga kujenga upya mahusiano mazuri baina ya wakulima na wakugaji kwani makundi haya yanahitajiana katika mahitaji na maisha ya kila siku kama ambavyo tumeona. Katika uzinduzi wa kampeni hii, Rais Samia aliwaita mbele wawakilishi kutoka upande na wakulima na wafugaji akawapatanisha kwa kuwaambia washikane mikono kama ishara ya kumaliza tofauti zao na kuanza ukurasa mpya wa maisha, kila mmoja akimtunza mwenzie kwani wanategemeana. _“Mlime, wanaolima na mfuge wanaofuga na kwamba tunategemeana wote. Ninyi ndiyo mnaotupa sisi uhai, mnatupa vitoweo, mnatupa na chakula, hakuna haja ya kugombana, hakuna haja ya kuuwana, wote ninyi ni wanadamu”_ anasisitiza Rais Samia.
Nimalizie kwa kusisitiza tena maeneo mengine ya nchi yetu kujifunza kwa Mvomero kwa kuwa na Kampeni ya Tutunzane na ikiwezekana ibebwe na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufanywa kuwa kampeni ya kitaifa, ikaboreshwa na kuwekewa muda maalumu kwani ina manufaa mengi sana na imegusa maeneo mengi ya kimaendeleo.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: 0620 800 462.