Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara amesema Serikali ya Tanzania inatekeleza mipango madhubuti ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa majini.
Prof. Kahyarara ameyasema hayo, leo tarehe 26 Agosti, 2024, wakati akifungua Mkutano wa 27 wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Ukaguzi wa Meli katika Bahari ya Hindi (IOMOU) wenye lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu juu ya ukaguzi meli zinazoingia katika bandari za nchi wanachama.
Prof. Kahyarara amesema kuwa Serikali imewekeza sana katika bandari hali inayochochea mageuzi makubwa ambayo imeanza kuleta matunda yenye tija kubwa ikiwemo kupungua kwa foleni ya meli kusubiri kutia nanga kutoka meli 40 hadi kufikia meli 18 kwa siku.
“Kwetu sisi Tanzania Bahari ya Hindi ni muhimu sana kwa sababu asilimia 98 ya biashara za nje zinapita katika Bahari hii ya Hindi”, amesema Prof. Kahyarara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amesema TASAC imefarijika kupata fursa ya kuratibu na kuandaa mkutano huu wa Kimataifa kwa nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi ambao unatoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu juu ya ukaguzi wa meli zinazoingia katika bandari za nchi wanachama.
“Wataalamu kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekutana kuanzia leo tarehe 26 hadi 30, Agosti, 2024 ili kujengeana uwezo wa namna bora ya kushirikiana katika kutekeleza makubaliano ya ukaguzi wa meli za kimataifa zinazoingia bandarini na kuimarisha udhibiti wa usalama, ulinzi wa vyombo vya usafiri na utunzaji wa mazingira majini,” amesema Bw. Salum.
Mkutano huo wa 27 wa IOMOU unafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo jijini Dar es Salaam, huku, takribani nchi 14 zinashiriki katika Mkutano huu ikiwemo mwenyeji Tanzania, Kenya, Msumbiji, Afrika Kusini, Madagasca, Msumbiji, Visiwa Usheli Sheli, India, Iran, Japan, Comoro, Myamar, Sri lanka na Australia.
Wakati huo huo, IOMOU, inaadhimisha miaka 25 tangu kuanzisha makubaliano hayo na Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi 6 za mwanzo kukubali kusaini Mkataba huu ambao kwa sasa kuna nchi zaidi ya 20 zinazoshirikiana katika kuutekeleza.
IOMOU inalenga kubaini na kutokomeza meli zilizo chini ya kiwango katika Bahari ya Hindi.