*************
Na Sixmund Begashe – Mtumba Dodoma
Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwaTanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii (REGROW), imeikabidhi Klabu ya Michezo ya Wizara ya Maliasili (Maliasili Sports Club) Jezi zitakazotumiwa na wanamichezo wa Klabu hiyo kwenye mashindano makubwa ya Idara na Taasisi za Umma (SHIMIWI) inayotarajiwa kufanyika Mwezi Septemba, Mkoani Morogoro.
Akiwa ameambatana na Maafisa wengine wa Mradi wa REGROW kukabidhi Jezi hizo, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa Mradi huo Bi. Mwajuma Diike amesema kuwa lengo kubwa la kuipatia Klabu ya Michezo ya Wizara ya Maliasili Jezi hizo ni ili kutangaza Utalii hususani kusini mwa Tanzania Pamoja na kuutangaza mradi kupitia michezo hiyo yenye mvuto mkubwa nchini.
Bi. Diike ameipongeza Klabu hiyo kwa kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye michezo mbalimbali na kutoa shime kwa wachezaji watakapo enda kwenye mashindano ya SHIMIWI wacheze kwa nguvu zote ili ishinde kwenye michezo yote.
Naye Mwenyekiti wa Klabu hiyo Bw. Gervas Mwashimaha, ameushukuru uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mradi wa REGROW kwa hamasa kubwa iliyotoa kupitia Jezi hizo na kuahidi kuwa Klabu hiyo haitakuwa na huruma kwa timu yeyote itakayo kutana nayo kwenye michezo hiyo ya SHIMIWI, wataishushia kipigo kikali cha kihistoria.