Timu ya mpira wa miguu ya kata ya Nyamhongolo imefanikiwa kuifunga timu ya mpira wa miguu ya waendesha pikipiki maarufu bodaboda magoli matatu kwa moja ikiwa ni muendelezo wa mashindano ya The Angeline Jimbo Cup msimu wa nane kwa mwaka 2024 yanayoendeshwa kwa ufadhili wa mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula (MNEC)
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliochezwa katika viwanja vya shule ya sekondari Buswelu, Nahodha wa timu ya kata ya Nyamhongolo Nemensi Leos amefafanua kuwa ushindi wao umetokana na kuzingatia maelekezo aliyoyatoa mwalimu wao kwa wachezaji mara baada ya kupoteza mchezo wao wa awali
‘.. Kufanikiwa kwetu kumetokana na kuyazingatia maelekezo tuliyopewa, Lakini kubwa zaidi tulipoteza mchezo uliopita hivyo kwa namna yeyote ilikuwa leo tucheze kwa nguvu zetu zote ili tuweze kushinda ..’ Alisema
Aidha nahodha huyo amemshukuru na kumpongeza mbunge wa jimbo la Ilemela kwa kuasisi na kuendelea na mashindano hayo kwa msimu wa nane mfululizo huku akiwataka wabunge wa maeneo mengine kuiga mfano huo
Nae kocha wa timu ya waendesha pikipiki maarufu bodaboda Pastansi Magilukas amefafanua kuwa wachezaji wake wamekosa matokeo mazuri sababu ya kuwa nje ya mchezo kwa siku ya leo na kwamba amewaahidi mashabiki wa timu yake kufanya vizuri katika mchezo unaofuata pamoja na kuwaomba kuzidi kujitokeza kuiunga mkono timu yao badala ya kukata tamaa
Mashindano ya The Angeline Jimbo Cup 2024 yanaendelea kila siku katika viwanja vinne vya jimbo la Ilemela vya Kona ya Bwiru shule ya Baptist, uwanja wa shule ya msingi Sabasaba, uwanja wa shule ya msingi Bugogwa na uwanja wa shule ya sekondari Buswelu huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Uchaguzi wa Serikali za mitaa, Ilemela tunaendelea tulipoishia’