WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kufungua mtandao wa barabara za vijijini katika wilaya ya Ruangwa ili ziweze kusaidia wananchi kusafirisha mazao yao.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 23, 2024) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namikulo, Kata ya Chunyu, wilayani Ruangwa, Lindi.
Amezitaja barabara hizo kuwa ni ya kutoka Namkatila, Matambalale A, Matambalale B Namikulo hadi Nangwego ambayo alisema imekwishafanyiwa tathmini na itaanza kujengwa mkandarasi akipatikana. “Barabara hii imeshafanyiwa tathmini na michoro iko tayari. Benki ya Dunia wanatafuta mkandarasi ili ifikapo Januari, 2025 kazi ya ujenzi ianze,” alisema.
Amesema barabara nyingine ni ya kutoka Ruangwa mjini hadi Namichiga yenye urefu wa km. 21 ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami. “Hii itajengwa na TANROADS kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Na sera ya sasa hivi, inataka barabara za lami zikipita kwenye vijiji, maeneo hayo yawekwe taa za barabarani ili wananchi waweze kufanya kazi za kujikimu. Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha hizo.”
Akielezea ujenzi wa barabara za vijijini ambazo si za lami, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kuimarisha barabara hizo na kutolea mfano barabara ya kutoka Chikwale hadi Machang’anja ambayo alisema hivi sasa inapitika bila shida.
Alisema awamu ya pili ya barabara hiyo itatoka Namichiga – Namkonjela – Nambilanje-Nanjalu- Kiperemende hadi Nanjilinji, wilayani Kilwa. Barabara hii ambayo imelenga kutoboa hadi wilaya nyingine ili kupanua wigo wa mawasiliano, bado haijapata fedha.
Alipotakiwa kutoa taarifa kuhusu barabara nyingine kwa wakazi wa kijiji cha Namikulo na vijiji jirani vya kata ya Chunyu, Meneja wa TARURA wa wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Nalupi alisema barabara ya kutoka Chunyu hadi Mihewe yenye urefu wa km.6 imetengewa sh. milioni 150 na itajengwa kiwango cha changarawe.
“Ipo barabara ya kutoka Chunyu hadi Namikulo ambayo imetengewa sh. milioni 10 kwa ajili ya kuichonga barabara hiyo na kujenga mifereji lakini pia kuna barabara ya kutoka Namilema hadi Matambarale ambayo itajengwa kwa kiwango cha udongo,” alisema.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa tatizo la maji, Meneja wa RUWASA wa wilaya hiyo, Mhandisi Lawrence Mapunda alisema wamekwishachimba kisima katika kijiji cha Liuguru chenye uwezo wa kutoa lita 10,500 kwa saa.
“Kisima kilichimbwa tangu Julai, 2024. Tayari tumetenga sh. bilioni 1.9 na sasa tunatafuta mkandarasi wa kusambaza maji hayo kwenye vijiji vinne vya Chunyu, Namikulo, Mihewe na Chiundu,” alisema na kusisitiza kuwa kazi hiyo inatarajiwa kuanza Oktoba, mwaka huu.