Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 23263/2024 lilifunguliwa Agosti 19, 2024 katika Mahakama ya Wilaya Ilala mbele ya Mhe. Battony Mwakisu-Hakimu Mkazi Mwandamizi, likihusisha washtakiwa watatu;
1.Flora Robert Urio (Mwalimu wa Shule ya Msingi Gerezani katika Halmashauri ya Manispaa Ilala)
2.Fidelis Casmir Shirima (Mjasiriamali) na
3.Edinister Issack Minja (Aliyekuwa Afisa Mikopo Kampuni binafsi ya PTF).
Wote walishtakiwa kutenda jumla ya makosa tisa (9) yakiwemo; Kughushi, Kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya Uongo kwa nia ya kumdanganya mwajiri, Kula njama na Kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Shilingi 53,227,555/=.
Washtakiwa Fidelis Shirima na Edinister Minja walikiri kutenda makosa hayo ambapo Mahakama iliwatia hatiani na kuhukumiwa kifungo cha nje kwa muda wa mwaka mmoja na kutakiwa kurejesha kiasi cha shilingi Milioni Kumi na nane (TSh.18,000,000) kila mmoja ndani ya mwaka mmoja tangu kutolewa kwa hukumu.
Aidha, mshtakiwa Flora Urio alikana kutenda makosa hayo na shauri limepangwa kusikiliza hoja za awali tarehe 25.09.2024.
Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana.
Shauri hili lilitokana na uchunguzi wa tuhuma ya kughushi na kutumia Cheti cha Ndoa inayodaiwa kufungwa baina ya Bi Flora Urio na Bw. Fidelis Shirima na hivyo kumwezesha Bw. Shirima kupata kadi ya mnufaika wa NHIF aliyoitumia kwa vipindi tofauti kupata matibabu mbalimbali na kusababisha NHIF kupata hasara ya shilingi 53,227,555/=.