Na Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Madini, Antony Mavunde amesema sekta ya madini katika mwaka wa fedha uliopita imeongeza fedha za kigeni zaidi ya asilimia 56 huku inaendelea kukua na kuongeza uchangiaji mapato ya taifa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2021/22 hadi kufika asilimia 9.0 mwaka huu.
Mavunde ameyasema hayo leo Agosti 21,2024 Jijini Dar es Salaam wakati akizundua maandalizi ya mkutano mkubwa wa kimataifa wa madini utakaofanyika nchini Novemba 19 hadi 21 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Akizungumzia ukuaji huo, Mavunde amesema mfano kwenye ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya madini kwa miaka sita iliyopita yalikuwa ni shilingi bilioni 168 hadi mwaka unafungwa wa fedha Juni 2023/24 maduhuli yaliyokusanywa na kwenda mfuko mkuu wa serikali yalikuwa sh bilioni 753.
“Sekta hii inakuwa kila siku na kuleta matumaini mapya, lakini ili kuongoza vizuri Watanzania na hasa wachimbaji wadogo na kuvutia sekta hii ni lazima tufanye utafiti wa kina na kuweza kubaini madini yetu kwa maana ya chini ya ardhi ili yawaongeze vizuri wachimbaji wadogo na wawekezaji,”amesema.
Aidha amesema kuwa serikali imefanikiwa kufanya utafiti wa jiolojia kwa asilimia 97 ila haijafanya utafiti wa kina na katika eneo hilo ambalo hadi sasa limefanyiwa utafiti wa asilimia 16 pekee.
“Tumefanya kwa asilimia 16 tu lakini ndani ya asilimia hizo ndio imefanya sekta hiyo katika mwaka wa fedha uliopita nchi imeongeza fedha za kigeni zaidi ya asilimia 56 kutokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi ambazo zilifika thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1’’,amesema Mavunde.
katika mapato ya kodi, Mavunde amesema kupitia sekta hiyo sh trilioni 2.1 zilikusanywa ambazo ni sawa na asilimia 15 ya mapato yote ya kodi iliyokusanywa.
Lakini pia, katika mwaka wa fedha ulioisha, katika vituo 100 vya ununuzi wa madini na masoko 42 ya madini fedha zilizozunguka katika sekta hiyo ilikuwa sh tirilioni 1.7 lakini pia manunuzi yaliyofanywa kwa mwaka huo yalifika zaidi ya sh trilioni 3.1.
“Kama tumefanya utafiti kwenye eneo la asilimia 16 na tukafika hatua hii,je tukifanya utafiti kwenye eneo kama hili mara mbili au tatu tutafikia wapi?,”amehoji Mavunde.
Hivyo amesema ndio maana wizara na serikali wamekuja na Dira ya 2030 ambayo inataka angalau wafike asilimia 50 ya eneo la utafiti kutoka asilimia 16 ya sasa.
Akizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Madini mwaka 2017, Mavunde amesema tangu yafanyike kuna mabadiliko makubwa.
“Tumeweka masharti magumu kwenye usafirishaji madini nje, ni lazima sasa uongeze thamani madini kabla ya kuyasafirisha, tumepata pia mwamko mzuri wa wadau lazima madini yaongezwe thamani hapa nchini,”amesema Mavunde.
Amesema wamejipanga mkutano huo uwe na manufaa kwa taifa na sekta ya madini huku akiwaomba wadau wa sekta binafsi kutumia fursa ya mkutano huo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kuchangamkia fursa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chemba ya Madini Tanzania , Benjamin Mchwampaka amesema mkutano huo umelenga kuhamasisha uongezaji thamani madini na utawashirikisha washiriki zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nchi mbalimbali duniani.
“Ni mkutano muhimu wa kunadi pia madini ya Tanzania na kufanya maonesho ya ya teknolojia za madini,uchimbaji na uchenjuaji ,Watanzania ni fursa kwao kuja kujifunza wengine wanafanya nini lakini pia wageni kujua fursa zilizopo nchini,”amesema Mchwampaka.