Na WAF – Meatu
Wakazi wa Wilaya ya Meatu wametakiwa kuboresha hali ya usafi wa vyoo na ndani ya siku saba kuwe na vyoo bora ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.
Wito huo umetolewa Agosti 20, 2024 kutoka kwenye maazimio ya Kikao cha Kamati ya Afya ngazi ya Msingi kilichofanyika Wilayani humo na kuongozwa na na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Prisca Kayombo na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe, Kamati ya Afya ya Wilaya, Madiwani, Viongozi wa Kata, Vijiji pamoja na Viongozi wa Dini.
“Kila kaya lazima iwe na choo, na baada ya siku saba, ifikapo tarehe 26/08/2024 atakayekutwa hana choo bora achukuliwe hatua” Amesema Bi. Prisca Kayombo Huku akiagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kusimamia zoezi hilo na kutoa taarifa ya utekelezaji kuwa Kaya ngapi zimejenga vyoo au kuboresha vyoo.
Kikao hicho kimepitisha maazimio saba yaliyolenga kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kipindukipindu ambao unakua ukitokea mara kwa mara Wilayani humo.
Azimio mojawapo ni kuhakikisha kanuni za afya zinafuatwa ikiwa ni pamoja na kujenga vyoo bora ndani ya siku saba hadi kufika tarehe 26 Agosti 2024, na atakayekutwa hana choo atachukuliwa hatua.
Aidha, kikao hicho kimepitisha azimio la utoaji wa elimu ya Afya juu ya umuhimu wa kunywa maji yaliyochemshwa au kuwekwa vidonge vya kutibu maji (AquaTabs) na viongozi wametakiwa kusimami zoezi la kuelimisha jamii na kuwatoa hofu na dhana potofu juu ya maji yaliyowekewa .
Maazimio mengine ni pamoja na wataalam kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wananchi ili kubaini uhifadhi wa vyakula, kusimamia usafi wa mazingira, Sungusungu kushiriki katika kusimamia usafi pamoja na kuwapa elimu waganga wa tiba asili ili waweze kubaini dalili za wagonjwa na kuwashauri wagonjwa kwenda Hospitalini kwa kwaajili ya kupata huduma matibabu.
Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hutokea mara kwa mara Wilayani humo huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni uchafu wa mazingira na vyanzo vya maji na kaya kutokua na vyoo bora.
Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo kwa kupeleka dawa (Aquatabs) pamoja an vifaatiba katika Mkoa wa Simiyu ili kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu