Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kufanya maboresho ya vifaa vya utabiri wa hali ya hewa ili kuwawezesha wataalam wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kufanya kazi kwa uweledi pamoja kuwajengea uwezo wanahabari katika kuhakikisha wanaripoti taarifa sahihi za hali ya hewa.
Akizungumza leo Agosti 21, 2024 jijini Dar es Salaam katika warsha na waandishi wa habari yenye lengo la kujadili namna bora ya kufikisha taarifa kwa wananchi kuhusu utabiri wa mvua za msimu wa Vuli zinazotarajia kuanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa taarifa za hali ya hewa ni muhimu katika kujipanga kwa kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Dkt. Chang’a amesema kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema ndani ya miaka mitano utabiri au masuala ya tahadhali ya hali ya hewa iwafikie watu wote duniani.
Amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi inayoongoza kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa ili kufika malengo ya kutoa taarifa sahihi za utabiri wa hali ya hewa.
“Usahihi wa msimu wa mvua za masika ni asilimia 98.4, usahihi huo umetokana na miundombinu ya uhakika ambayo imewekezwa na Serikali ya Awamu ya Sita” amesema Dkt. Chang’a.
Dkt. Chang’a amesema kuwa kutokana na uwekezaji uliofanyika wameweza kutoa huduma ya utabiri wa hali ya hewa Wilaya 86 katika maeneo madogo madogo.
Amesema kuwa lengo kufikisha taarifa sahihi za hali ya hewa pamoja na athari zake kutokana zina umuhimu mkubwa ikiwemo kupanga utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii.
Mwelekeo wa msimu wa Vuli 2024 unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2024 ambao umebeba kauli mbiu isemayo : Matumizi sahihi ya hali ya hewa kwa wote na wakati.