ABUJA, Nigeria – Agosti 21, 2024 –
Makamu wa Rais wa Nigeria Mhe. Kashim Shettima ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Nigeria na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa kikanda na juhudi za pamoja ili kufanikisha ukuaji na umoja wa bara.
Alitoa maoni haya Jumanne wakati wa mkutano na Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, katika Ikulu ya Rais, Abuja.
Akizungumzia uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili, Makamu wa Rais Shettima alibainisha kwamba nchi zote mbili zina uhusiano wa muda mrefu, hasa kama nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukoloni.
Alisisitiza haja ya kujenga juu ya historia hii ya pamoja ili kukuza uhusiano imara wa kiuchumi na kijamii, hasa ndani ya mfumo wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
“Tanzania ni moja ya hadithi za mafanikio za Afrika,” alisema Shettima, akilipongeza Taifa hilo kwa uongozi wake. “Kuanzia Julius Nyerere hadi Samia Suluhu Hassan, Tanzania imebarikiwa na viongozi bora. Taifa hili ni mfano wa matumaini na utulivu katika Afrika Mashariki.”
Makamu wa Rais huyo wa Nigeria alionesha furaha kwa kugundulika kwa akiba kubwa ya gesi, akisema kuwa Tanzania iko kwenye njia ya maendeleo ya haraka, jambo ambalo linafungua fursa za ushirikiano wa kina kati ya mataifa haya mawili.
“Iwapo mataifa muhimu ya Afrika kama Nigeria na Tanzania yatapata mafanikio, bara zima litanufaika,” aliongeza.
Mhe. Shettima pia aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono biashara za Nigeria zinazofanya kazi ndani ya mipaka yake, akitaja mafanikio ya kampuni kama United Bank for Africa, Guarantee Trust Bank, na Dangote Group.
Alisisitiza uwezekano wa kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili, jambo ambalo litazidi kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi.
Akijibu, Rais wa zamani Kikwete alielezea utayari wa Tanzania kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na kidiplomasia na Nigeria, na kwamba anatambua umuhimu wa urafiki kati ya mataifa haya mawili na akasisitiza dhamira ya Tanzania ya kuzidisha uhusiano huo.
“Tunathamini urafiki na ushirikiano kati ya Nigeria na Tanzania na tumejizatiti katika kuuzidisha zaidi,” alisema Kikwete.
Mhe. Kikwete pia alitambua jukumu la Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria katika kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Tanzania, akibainisha kuwa ushirikiano huu ni sehemu muhimu ya uhusiano wa ulinzi na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, akieleza kuridhishwa kwake kwa ushirikiano wa kina na mpana katika maeneo haya.
Viongozi wote wawili walikubaliana juu ya umuhimu wa kuangalia upya na kusahisisha mikataba ya kibiashara iliyopitwa na wakati ili kuendana na hali halisi za sasa na kukuza uhusiano wao kwa mshikamano wa Afrika.
Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana na Makamu wa Rais wa Nigeria Mhe. Kashim Shettima
katika Ikulu ya Rais, Abuja.
Mkutano huo ulihudhuriwa na maafisa muhimu, wakiwemo Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Bi. Judica Nagunwa; Mkurugenzi wa Masuala ya Kitaifa na Kijiografia katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria, Balozi Akin Oyateru; mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, Ahmed Baba Mohammed; na Katibu Binafsi wa Rais wa zamani wa Tanzania, Medard Ngaiza.