Na Neema Mtuka, RUKWA
Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) Mkoani hapa wamesema wanaendelea kununua mahindi katika vituo vyake vya ununuzi wa mazao katika maeneo mbalimbali sambamba na kutumia mizani ya mifumo ya kidigitali kwenye ununuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meneja wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) mkoa wa Rukwa Marwa Range amesema lengo ni kutaka kuwarahisishia wakulima kuuza mazao yao kwa urahisi na bila bugudha.
Amesema katika vituo hivyo wanatumia mizani ya kidigitali kupima uzito wakati wa kununua nafaka kutoka kwa wakulima mkoani humo.
“Tumepanga kununua zaidi ya tani 100,000 za nafaka ,wakulima walete mahindi yaliyokauka na yasiyo na unyevu ,wafike ofisini ili kuepuka udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu kwa sababu sisi hatutumii madalali katika ununuzi wa nafaka ,”Amesema Range.
Aidha amesema kuwa vituo vyote vinatumia mizani hiyo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kazi ya ununuzi wa nafaka na kupunguza malalamiko.
“Wafanyabiashara wakubwa na wakulima wote hasa wadogo wasisite kuleta nafaka zikiwa safi maana tumepanga kununua mahindi meupe katika msimu huu wa ununuzi hivyo wahakikishe wanaleta nafaka hizo katika ubora unaotakiwa,”Amesema Range.
Baadhi ya wakulima waliopeleka mazao yao akiwemo Albert Kaozya ameuomba wakala huo kulipa fedha kwa wakati.
Hata hivyo Meneja Range amewatoa hofu wakulima kuwa hakuna atakayekopwa .,”Kila mkulima atalipwa kwa wakati ,hatutarajii kumkopa mkulima yeyote.” Amesema Meneja huyo.
Amesema vituo ambavyo vinaendelea na zoezi la kununua mazao kwa msimu huu wa ununuzi kwa Sumbawanga ni Mazwi Kanondo na Laela.
kwa wilaya ya Kalambo ni pamoja na kituo cha Mwimbi Matai na Mkombo huku wilayani Nkasi ni Namanyere Mtenga ,Kasu na Ntalamila .