Na Neema Mtuka, Rukwa
Wananchi Mkoani Rukwa wametakiwa kuachana na mawazo potofu kuwa uwekezaji ni kwa ajili ya watu wa nje na badala yake wachangamkie fursa za uwekezaji.
Hayo yamesemwa na Meneja wa kituo Cha Uhamasishaji na uwekezaji wa ndani (TIC) Felix John wakati akizungumza katika kiwanda Cha samaki Cha Alpha.
Amesema kuwa wamefika Mkoani Rukwa lengo ni kubadili fikra za wananchi kuhusu uwekezaji kuwa sio kwa ajili ya wageni bali hata wao Wana nafasi kubwa ya kuwekeza.
“Wananchi wengi wanafikiri kuwa suala la uwekezaji sio la kwao wanaona kama hayo mambo ni kwa ajili ya watu wa nje jambo ambalo sio kweli hata watanzania wanayo nafasi kubwa ya kuwekeza.”Amesema Meneja.
Kwa upande wake afisa mwekezaji wa nyanda za juu kusini Privata Simon amewasihi wanawake na vijana kujitokeza kusajili miradi kwa kuwa kwa Sasa Sheria imeboreshwa.
Ameongeza kuwa hapo nyuma makundi hayo yalishindwa kujisajili kutokana na Sheria zilizokuwepo na hata wao kutochangamkia fursa hiyo.
Baadhi ya vijana wanaofanya kazi katika kiwanda Cha samaki Cha Alpha akiwemo Lazaro kusula amesema hapo nyuma Sheria za usajili zilikuwa zinawabana lakini kwa Sasa wataunda vikundi ili kusajili miradi yao.
“Vijana wengi wanatamani kusajili ili kufanya kazi kisheria lakini wanashindwa kutokana na michakato kuwa mingi.”Amesema kusula.
Kwa upande wake mwekezaji katika kiwanda Cha samaki Alpha ya Mungu ameiomba Serikali kutenga maeneo kwa ajili ya watu mbalimbali kuweza kuwekeza.
Kampeni ya Uhamasishaji wananchi katika uwekezaji inafanyika nchi nzima Ambapo lengo lake ni kuwahimiza wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo Nchini.