Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma (Mwana FA) akitoa burudani baada ya kuzindua Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yaliofanyika Agosti 19, 2024, Msasani Beach, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma (Mwana FA) akizungumza jambo katika hafla ya Uzinduzi Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yaliofanyika Agosti 19, 2024, Msasani Beach, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, akizungumza jambo katika hafla ya Uzinduzi Mashindano hayo yaliofanyika Agosti 19, 2024, Msasani Beach, Dar es Salaam.
Picha za matukio mbalimbali katika hafla ya ufunguzi wa Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yaliofanyika Msasani Beach Jijini Dar es Salaam Agosti 19, 2024
……..
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma amefungua mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi ambapo amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hususani Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Jacob John Mkunda kwa kuja na wazo la kuwa na mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi (CDF Cultural Competition).
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo yaliofanyika Msasani Beach Jijini Dar es Salaam Agosti 19, 2024 Mhe. Mwinjuma amesema kuwa Jeshi limetekeleza kwa vitendo maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu kuwa kila mmoja ana wajibu wa kupenda, kuenzi na kuendeleza utamaduni wetu.
“Nimefurahi sana kusikia kuwa mashindano haya yatakuwa yanafanyika kila mwaka lakini kwa mwaka huu ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 60 ya Jeshi letu. Jambo hili ni la msingi sana kwa uhai wa taifa letu na ukweli Jeshi limeandika historia kubwa ”
Mhe. Mwinjuma ameonesha kupendezwa na mwamko wa vikundi vya sanaa vya Jeshi kushiriki mashindano hayo pia ambavyo jeshi limeweza kuwa na bendi na vikundi vya ngoma vingi ambavyo kipekee vinadumisha na kuendeleza utamaduni.
“Kufanyika kwa mashindano haya kwetu imekuwa ni faraja kubwa, niahidi hapa kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Dkt.Damas Ndumbaro kuwa Wizara itatoa kila aina ya msaada unaotakiwa kuhakikisha mashindano haya muhimu yanafanikiwa”
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ.
“Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda ameaona ni vyema baada ya kuona sanaa na utamaduni vinapotea, hivyo ameruhusu kuwa vikundi vya ngoma za asili kwa mfumo wa mashindano” Meja Jenerali Mkeremy.
Meja Jenerali Mkeremy amesema kuwa mashindano haya yatakuwa endelevu ambayo yatafanyika kila mwaka, huku akieleza kwa mwaka huu Kuna bendi 10 za muziki wa dansi na vikundi vya ngoma za asili ambavyo vitashindanishwa.
Meja Jenerali Mkeremy amesema katika kufanikisha mashindano hayo wameshirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), huku akieleza kuwa washiriki wote watapewa zawadi, huku washindi watapata fursa ya kurekodiwa video na audio na na kupata nafasi ya kutoa burudani kwenye Kilele miaka 6 ya JWTZ .