Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere wakati akifungua rasmi semina ya uwekezaji
Meneja Uhamasishaji uwekezaji wa ndani kituo Cha uwekezaji Tanzania wakati akitoa wasilisho la fursa za uwekezaji.
…………….
Na Neema Mtuka, Rukwa.
Wananchi Mkoani Rukwa wametakiwa kutumia vivutio mbalimbali vilivyopo katika mkoa huo kwa lengo la kujiingizia kipato.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere katika semina ya uwekezaji kwa wafanyabiashara na wajasiriamali sambamba na wawekezaji iliyofanyika katika Ukumbi wa mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Makongoro amewataka wawekezaji wa ndani kujenga viwanda pamoja na hoteli katika mwambao wa ziwa Tanganyika pamoja na ziwa Rukwa Ambapo huko kote Kuna vivutio na wananchi wengi watapata ajira.
Ameongeza kuwa vivutio vya kikodi ambavyo Serikali imetoa vitawanufaisha wawekezaji wa ndani ambao wamekuwa ni waoga kuthubutu kuwekeza .
Awali akiwasilisha wasilisho la fursa za uwekezaji Meneja wa kituo Cha Uhamasishaji uwekezaji wa ndani TIC Felix John amewasihi wajasiriamali kusajiri miradi yao ili kunufaika na vivutio vya kikodi vilivyofanyiwa marekebisho ili kumfikia Kila mwekezaji.
“Maboresho ya Sheria ya Kodi pamoja na vivutio vyake yamewarahisishia wawekezaji wa ndani kuwekeza na kunufaika na vivutio vya kikodi .”Amesema Felix
Aidha amesema kuwa wao wamejikita katika kuhamasisha na kusaidia kupatikana kwa vibali na leseni mbalimbali wanazozihitaji kusajili na kutekeleza miradi , sambamba na kuishauri Serikali kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusiana na sera ya uwekezaji Nchini.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara Willington Kiziba amesema watatumia fursa zilizopo kwa kuwa vizuizi ambavyo ni vikwazo vimeondolewa.
Amesema hapo nyuma walikuwa wakiogopa kuwekeza kutokana na Sheria kuwabana na kuwepo kwa michakato mingi.
Kwa upande wake Afisa mwekezaji wa Kanda ya nyanda za juu kusini Privata Simon amesema lengo la kampeni hiyo ambayo inaendelea nchi nzima ni kuongeza fursa za ajira mpya kwa vijana na kuongeza mapato yatokanayo na Kodi na yasiyo ya kikodi.
Nao baadhi ya washiriki wa semina hiyo akiwemo Nicholas mwemenzi wamekipongeza kituo hicho Cha uwekezaji na kusema kuwa maboresho ya Kodi yamewapa nafasi ya kuwekeza bila uoga.
TIC imepewa jukumu na Serikali la kusimamia dira kwa kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda.