Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa, amewataka wajasiriamali wa Mkoa huo kuwa na matumizi bora ya fedha wanazozipata katika shughuli zao mbalimbali za uzalishaji mali ili kuepukana na mikopo isiyo rasmi (mikopo umiza).
Dkt. Mussa alisema hayo wakati wa kikao na timu ya kutoa elimu ya fedha kwa Umma kutoka Wizara ya Fedha ambayo ipo Mkoani Morogoro kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya wananchi katika halmashauri saba (7) za Mkoani wa Morogoro.
‘’Shida moja niliyoigundua kwa wananchi wetu wa Morogoro wanaweza wakapewa mkopo, na pengine hawana haja ya kupewa mkopo kutokana na kipato chao, lakini kipato chenyewe kinatumika vibaya na kikitumika vibaya inawasababishia kuwa na mikopo isiyotarajiwa hasa ile ya kinyonyaji’’ alisema Dkt. Mussa.
Dkt. Mussa aliwataka waratibu wa program ya elimu hiyo pamoja na yale waliyokusudia kuwaelimisha wananchi kuhusu program ya utoaji elimu ya masuala ya fedha, wakumbuke pia kuwaelimisha kuhusu matumizi ya rasilimali walizonazo ambazo zitawasaidia kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuwaepusha na mikopo ya kinyonyaji.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kupitia kikao hicho aliwaasa wananchi wa Halmashauri zitakazotembelewa na timu kuhakikisha hawakosi fursa hiyo ya kupata elimu ya masuala ya usimamizi wa fedha binasfi, uwekaji wa akiba, mikopo na mengineyo ambayo itawasaidia katika maisha ya baadaye.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa lengo la Wizara kutoa elimu hiyo ni kujaribu kuwahiza wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha pesa wanayoipata kutokana na uzalishaji mbalimbali wanaoufanya wanaiwekeza kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Aidha, Bw. Kibakaya aliongeza kuwa program ya elimu ya fedha italenga pia watoa huduma ya fedha kwa kuwahimiza kutoa huduma hizo kwa kufuata sheria na miongozo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ambazo hazijajirasimisha kufanya hivyo ili wapatiwe leseni itakayowawezesha kufanya shughuli za utoaji wa huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia sheria.
Programu ya kutoa elimu ya Fedha kwa umma Mkoani Morogoro itafanyika katika Halmashauri ya Morogoro Mjini, Morogoro vijijini, Kilosa, Mvomero, Ifakara, Mlimba na Gairo.