Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
20, Agosti,2024
HALMASHAURI Mkoani Pwani zimetakiwa kutumia fedha zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe kama zilivyopangwa pamoja na kutenga fedha za vibao vya ufuatiliaji wa makuzi ya watoto katika kila kituo.
Ofisa lishe Mkoani Pwani, Mecy Mtaita akitoa taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 alieleza mikakati waliyojiwekea ili kuweza kufikia malengo ya mkataba wa lishe.
Alisema, baadhi ya halmashauri zimekuwa zikishindwa kutumia fedha kulingana na mipango hivyo kuathiri ubora wa utekelezaji.
“Kati ya halmashauri zote halmashauri zilizofanya vizuri kupunguza fedha pangwa na matumizi ya fedha za lishe ni Kibaha Mjini na Kisarawe kwa asilimia 100 na Kisarawe 99.5.” alieleza Mtaita.
Kadhalika , alifafanua kumekuwa na upungufu wa vibao vya ufuatiliaji wa makuzi ya watoto ,ambapo kibao kimoja kinapatikana kwa bei ya sh.250,000-350,000.
“Hakuna takwimu katika kufanya maamuzi katika udumavu na ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano, kwakuwa hakuna vitendea kazi vya kusaidia kufanya tathmini hizo kwenye vituo vya kutolea huduma “
“Ili waweze kupima lazima wawe na vibao ,kwasasa kuna asilimia 27 ya vibao na lengo kila kituo kufanya tathmini kwa watoto ili kuchukua hatua mapema ikihitajika”alieleza
Pamoja na hayo, Mtaita alieleza kuna changamoto ya idadi ndogo ya wanafunzi wanaonufaika na huduma ya chakula shuleni na mkoa kuwa na shule chache zinazotumia unga ulioongezewa virutubishi.
“Uhamasishaji na ushirikishwaji wa bodi za shule ,wazazi na viongozi wa mtaa,vijiji wahakikishe chakula kinapatikana shuleni “
Alieleza, maboresho ya mipango na bajeti za lishe yanahitajika ili kuakisi uhitaji wa jamii kuongeza upatikanaji huduma za kutosha za lishe zenye ubora na kwa usawa.
Mtaita anasisitiza pia kuwajengea uwezo watendaji wa serikali za mitaa, wahudumu ngazi ya jamii na afya ili kutekeleza shughuli za lishe sanjali na kuendana na mpango mkakati wa kitaifa wa lishe.
Alitaja changamoto ya mkoa kuwa na shule chache zinazotumia unga ulioongezewa virutubishi na ukosefu wa iodine test kits kwa muda mrefu hivyo kuathiri upimaji wa uwepo wa madini joto kwenye chumvi zinazotumiwa na wanajamii.
Kutokana na hilo,Ofisa lishe huyo alieleza wakurugenzi wanapaswa kuelekeza na kusimamia viwanda vyote vinavyosindika unga wa mahindi kufungiwa na kutumia mashine zinazorutubisha unga.
Alieleza halmashauri zinazozalisha chumvi kutumia maabara za halmashauri kupima uwepo wa madini joto katika maeneo yote ya uzalishaji sambamba na kutumia wadau kutengeneza bidhaa zenye virutubishi vingi.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alisisitiza z halmashauri kutoa fedha kwa wakati katika kutekeleza masuala ya lishe.
Aliomba viongozi na watendaji kushirikiana kufanya kazi ili kuinua maendeleo na Uchumi wa mkoa kwa umoja.