NA FAUZIA MUSSA
TAASISI ya ‘Together for Samia’ imesema inaendelea na mikakati ya kuelezea utendaji kazi wa viongozi wakuu wa Nchi ili jamii itambue na kuthamini juhudi za viongozi hao.
Mwazilishi wa Taasisi ya hiyo Slim Salim Mohammed ameyasema hayo katika hafla ya kutoa ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dk. Samia Suluh Hassan kwa njia ya makachu huko Forodhani Mjini Unguja.
Alisema utendaji kazi wa kiongozi huyo unamgusa kila mtu wakiwemo vijana , jambo ambalo alilitaja kuwasukuma kuanzisha taasisi hiyo ili kuzielezea juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi kwa jamii, Taifa na Dunia kwa ujumla.
“Dk. Samia anafanya vizuri katika Sekta zote, ikiwemo afya, elimu, miundombinu na hata demokrasia jambo ambalo linaleta Amani katika Nchi yetu.” alisema Slim
Aidha alieleza kuwa Taasisi hiyo imeamua kuwatumia Vijana wa makachu kufanikisha hafla hiyo ili ujumbe unaotolewa kufika kwa wananchi wa Tanzania na dunia kwa ujumla kwa haraka zaidi.
Vilevile alisema hivi karibuni Taasisi hiyo itazielezea na kuonesha shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ikiwa ni sehemu ya kutambua jitahada anazozichukua kiongozi huyo katika kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo vijana.
Miongoni mwa wananchi walioshuhudia hafla hiyo Massoud Salim Mohammed alisema hatua ya vijana hao kuanzisha na kuendesha taasisi hiyo kwa gharama zao kunaonesha wazi mapenzi waliyonayo kwa viongozi wa nchi pamoja na kuthamini juhudi za kimaendeleo za viongozi hao.
Alieleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na viongozi makini, na mahiri wenye mapenzi na wanachi wao waliojitoa kuendesha nchi bila kujali maslahi binafsi, hivyo kuna kila sababu ya watanzania kutambua na kuthamini juhudi hizo.
Kwa upande wake Mwazilishi wa Makachu Jamal Amour Abdalla alisema wanafurahishwa kuona Sanaa yao inaendelea kutumika katika kufikisha ujumbe wa matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Aidha aliziomba Serikali zote mbili kuwasaidia wasanii hao kupata bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote.
Hatahivyo waliomba Serikali na wadau wa Sanaa hiyo kuweka kituo cha huduma za dharura katika eneo wanaloendeshea shuguli zao pamoja na gari la kubebea wagonjwa ili kusaidia kuwahi kituo cha afya pale madhara yanapotokea.
Miongoni mwa ujumbe uliotolewa na vijana wa ‘together for Sami’ kwa njia ya makachu ni pamoja na “mama tunakupenda, tunakuthamini na tutakulinda, muumini wa maridhiano, kipenzi cha wengi, anaimarisha uchumi na kuipaisha Tanazania siku hadi siku , Mjenzi wa Demokrasia.”