Meneja wa TARURA Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mhandisi Silvanus Ngonyani,akitoa taarifa ya hali ya barabara zinazosimamiwa na Tarura kwenye hafla fupi ya kutambulishwa wakandarasi waliopata kazi ya ujenzi wa miradi ya barabara wilayani humo,kulia Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha,aizungumza na watumishi wa Tarura na Wakandarasi waliopata kazi ya ujenzi wa miradi ya barabara zilizo chini ya Tarura wilayani humo,kushoto meneja wa Tarura Mhandisi Silivanus Ngonyani.
…………………
Na Mwandishi Maalum,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Simon Chacha,amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara wilayani humo kuzitendea haki fedha zinazotolewa na Serikali kwa kujenga miradi yenye viwango itakayosukuma na kuharakisha shughuli za maendeleokwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Chacha amesema hayo jana,wakati akizungumza na watumishi wa Tarura na wakandarasi waliopata kazi za ujenzi wa miradi ya barabara zinazosimamiwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA)wilayani humo.
Dc Chacha,amewaeleza wakandarasi hao kutekeleza kazi zilizoko kwenye mikataba waliyoingia na Serikali kupitia Tarura,kuwa wazalendo kwa nchi yao na kujenga miradi yenye viwango ambayo itachochea na kuharakikisha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya na Taifa.
“nendeni mkapige kambi kwenye maeneo ya miradi ili mpate muda mwingi utakaowawezesha kukamilisha kazi mlizopewa kwa wakati, wananchi wana matarajio makubwa na nyinyi, epukeni kuwa na visingizio vinavyoweza kuchelewesha ujenzi wa miradi,kazi zenu zitakwenda kuongeza thamani na ubora wa maeneo husika na zitasaidia wananchi kupata huduma bora za kijamii”alisema Chacha.
Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Silvanus Ngonyani alisema,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Tarura Wilaya ya Tunduru,imeidhinishiwa Sh.bilioni 4,110,783,784.47 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo mfuko wa Jimbo,tozo ya ushuru ya Sh.100 kwa lita moja ya mafuta na fedha za mfuko Mkuu wa barabara.
Alisema,katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa bajeti ya 2024/2025 jumla ya mikataba 11 yenye thamani ya Sh.2,807,981,498.00 imesainiwa kati ya mikataba hiyo,mikataba 4 ni ya vikundi maalum ya wanawake,vijana na wenye ulemavu na mikataba 7 ni kandarasi za kawaida.
Alisema,fedha hizo zitatumika kujenga makalavati 7,kufanya matengenezo ya barabara za udongo zenye urefu wa kilometa 109.8,barabara za changarawe kilometa 70 na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 1.67.
Ngonyani alisema,Tarura Wilaya ya Tunduru ina mtandao wa barabara wenye kilometa 1,203.61 kati ya hizo kilometa 360.56 ni za mjazio,kilometa 841.65 ni za mkusanyo na kilometa 1.4 ni za jamii.
Alisema kuwa, barabara katika wilaya ya Tunduru imegawanyika kwenye makundi makuu matatu ambapo kilometa 348.74 ni barabara za changarawe,kilometa 8.218 barabara za lami na kilometa 846.652 za udongo.
Pia alieleza kuwa,mtandao wa barabara za lami na changarawe hupitika kirahisi majira yote ya mwaka na barabara za udongo hupitika kwa shida wakati wa mvua.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa(TAKUKU)Wilayani humo George Njoholo, amewataka wakandarasi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango ili iendane na gharama halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.
“sisi kama Takukuru tutafika na kufuatilia kila mradi unaokwenda kutekelezwa kwa fedha hizi,nawaomba sana mkatimize wajibu wenu ili wananchi wazitumie barabara hizo kwenye shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo”alisema Njoholo.
Mwakilishi wa Wabunge wa wilaya ya Tunduru Hamad Seif alisema,miradi inayokwenda kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 itasaidia sana upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwa wananchi wa majimbo mawili ya Tunduru Kaskazini na Tunduru Kusini.
Amewaonya,kuepuka kuzalisha migogoro kati yao na jamii kwa kupitisha miradi bila kuwashirikisha wananchi na viongozi wa maeneo husika.