Askari Magereza wakishiriki matembezi ya hiari yaliyoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa (hayupo pichani, leo.
Maofisa,Wakaguzi na Askari Polisi , Magereza, Uhamiaji na Zimamoto, wakinyoosha viungo baada ya kuhitimisha matembezi ya hiari katika uwanaj wa Polisi Mabatini ,leo.
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Naibu Kamishna wa Polisi( DCP), Wilbrod Mutafungwa ameongoza vyombo vya usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mkoani humu kufanya matembezi ya hiari (route match) katika mitaa ya Jiji.
Matembezi hayo yaliyofanyika leo Jumamosi Agosti 17,2024, yamejumuisha askari wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji mkoani humo.
Mazoezi hayo ya pamoja yanalenga kuimarisha ushirikiano wa askari, utimamu wa miili na akili katika kutekeleza majukumu ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Mutafungwa amesema mbali na kuongeza ari katika utekelezaji majukumu ya ulinzi na usalama, yanaongeza ushirikiano baina yao huku akiwapongeza askari walioshiriki matembezi hayo.
“Mazoezi haya yatatusaidia kufahamiana,hivi karibuni tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na watu wanategemea usalama siku za kupiga kura, wakati wa kampeni na wakati wa kupeleka vifaa katika vituo vya kupigia kura,” amesema DCP Mutafungwa.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Ramadhan Ngoi kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Justine Kaziulaya amesema mazoezi ni muhimu kwa afya na kuwashauri kwa askari kuyazingatia na kushiriki kikamilifu.
Naye, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Ilemela,Deus Ruta ameshauri mazoezi hayo yawe endelevu miongoni mwa askari wa majeshi hayo.
Aidha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Mwanza (SACI), Colla Kayumba amesema kulingana na majukumu yanayofanywa na vyombo hivyo kuna umuhimu wa kufahamiana na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu.