MBUNGE wa jimbo la Mahonda Abdallah Ali Mwinyi , akiwahutubia Wananchi wa Wadi ya Kiwengwa katika hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali kwa wananchi vikiwemo mitungi ya gesi, mabati ya kuezekea nyumba, matangi ya kuhifadhi maji,mipira ya kusambaza maji ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
MBUNGE wa jimbo la Mahonda Abdallah Ali Mwinyi,akikabidhi mitungi ya gesi kwa kikundi cha ujasiriamali cha Baba na Mamalishe kilichopo Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
MBUNGE wa jimbo la Mahonda Abdallah Ali Mwinyi,akikabidhi mipira ya kusambaza maji kwa uongozi wa Jimbo la Mahonda katika hafla ya kugawa vitendea kazi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025
………..
NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
MBUNGE wa jimbo la Mahonda Abdallah Ali Mwinyi, amesema wajibu wa viongozi wa majimbo ni kuisaidia serikali katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na miradi mbali mbali ya maendeleo, ili kutatua changamoto za wananchi wake.
Aliyasema hayo katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi 150 kwa mama lishe na baba lishe, vifaa vya maji kwa wananchi wa shehiya ya Kilombero, mabati kwa madrasa ya Matetema na Mahonda, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM 2020/2025, iliyofanyika huko Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema anatambuwa kuwa katika jimbo hilo kuna changamoto nyingi ambazo zinawakabili na serikali imekuwa ikijitahidi kufanya kila juhudi kukabiliana nazo na kuwaletea wananchi wake maendeleo ili kuona wananchi wake wanaishi katika mazingira bora.
Hivyo alisema kwa kuwa serikali inafanya hivyo ni wajibu wao kama viongozi wa majimbo kuhakikisha zile sehemu ambazo hawajazifikia kusaidia.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na maji safi na salama, afya, elimu na barabara za ndani, ambazo kwa muda mfupi itakuwa ni historia.
Akizungumzia kundi la mama lishe na baba lishe alisema ni kundi ambalo linahitaji kupata usaidizi ili kuendesha shughuli zao za kuendelea kujiajiri wenyewe.
Hivyo aliwataka kujikusanya na kujisajili huku ofisi yake itajitahidi kutafuta na kubuni njia mbali mbali za kuhakikisha wanawapatia mikopo ili kupambana na tatizo la ajira nchini.
Alisema kuwa akiwa kama kiongozi amekuwa akitatua baadhi changamoto kwa hatua ndani ya jimbo hilo, ili kuona wananchi wake wanafaidika na matunda ya mapinduzi.
Kuhusu ajira alisema hilo ni tatizo kubwa duniani na serikali hata ifanye vipi haiwezi kulimaliza, hivyo wajibu wao washirikiane ili waweze kujiajiri wenyewe.
Mapema Katibu wa Jimbo hilo Simba Haji Mcha, alitoa shukurani zao kwa mbunge huyo kwa adhma yake ya kutoa msaada huo.
Alisema kitendo ambacho amekifanya ni mwendelezo wake katika kuhakikisha anatekeleza kwa vitendo ilani ya chama ambayo alikabidhiwa na kuja kuifanyia kazi.
“Tunamshukuru kiongozi wetu huyu leo ametoa msaada huu kwa mama lishe na baba lishe lakini katika siku za mbele atatuma kwa makundi mengine”, alisema.
Sambamba na hayo aliwataka akinamama lishe na baba lishe waendelee na moyo walio nao wa kuimarisha maendeleo yao katika jimbo.
Katibu wa Vijana CCM Wilaya ya Kaskazini B, Ashura Mohammed Ali aliwataka kuvitumia vyema na kuwa waangalifu katika vifaa hivyo ambapo kinyume na hilo vitawaangamiza.
Wakitoa shukrani zao mama lishe na baba lishe waliomba kupatiwa mafunzo ya matumizi ya majiko hayo ili kuepusha hasara.
Aidha waliomba kupatiwa hati za usajili kwa vikundi vyao ili kuweza kujiendeleza na kuweza kupata mikopo kwa haraka.
Walisema kuwa wananchi wamehamasika sana kujiunga na vikundi vya ushirika lakini changamoto kubwa ipo katika usajili na kupatiwa hati za usajili wa vikundi hivyo, ambazo zinapelekea kushindwa kufikia malengo yao.